Na Chikoti Cico
Baada ya timu ya Newcastle United kuitoa Manchester City kwenye raundi ya nne ya Capital One Cup kwa kuifunga kwa magoli 2-1, wanarejea tena kwenye uwanja wao nyumbani wa St James Park kuikaribisha timu ya Liverpool katika mfululizo wa mechi za ligi kuu ya Uingereza, mchezo utakaopigwa saa 9:45 kwa saa za Afrika Mashariki.
Kocha wa Newcastle United, Alan Pardew ambaye alikuwa hatarini kufukuzwa kazi baada ya timu kuwa na mwenendo mbaya, ataingia kwenye mchezo huo kutafuta alama nyingine tatu baada ya kushinda michezo miwili mfululizo ya ligi dhidi ya Leicester City na Tottenham Hotspurs, ushindi uliofufua matumaini ya ajira ya Pardew kutokuota mbawa.
Newcastle United ambayo inashika nafasi ya 14 ikiwa na alama 10 kati ya michezo tisa iliyocheza kwenye ligi, inatarajiwa kumkosa kiungo Cheick Tiote ambaye ni majeruhi huku mshambuliaji Papiss Cisse, akiwa na hati hati ya kucheza mchezo huo kutokana na kuumia goti.
Wakati huo huo, beki wa katikati Mike Williamson anatarajiwa kutokucheza ili aweze kuwa fiti zaidi baada ya kuwa na matatizo ya misuli.
Takwimu zinaonyesha katika michezo minne iliyopita ya ligi dhidi ya Liverpool, Newcastle imeweza kushinda michezo miwili na kutoka sare mchezo mmoja huku ikifungwa mchezo mmoja.
Wachezaji wa tano wa Newcastle walipewa kadi nyekundu katika michezo hiyo minne.
Kikosi cha Newcastle kinaweza kuwa hivi: Krul; Janmaat, Taylor, Coloccini, Dummett; Anita, Colback; Gouffran, Sissoko, Ameobi; Perez
Liverpool inayofundishwa na kocha Brendan Rodgers, itaendelea kuwakosa mshambuliaji Daniel Sturridge, mabeki Mamadou Sakho, Jose Enrique pamoja na Jon Flanagan ambao wote ni majeruhi.
Hivyo katika kumkosa Sturridge, kocha Brendan anatarajiwa kumwanzisha Mario Balotelli kuongoza safu ya ushambuliaji ya Liverpool.
Timu ya Liverpool ambayo inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 14 katika michezo tisa iliyocheza, inahitaji kushinda mchezo huo dhidi ya Newcastle ili kujitengenezea mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi ya kuwa kati ya timu nne za juu (top four).
Takwimu zinaonyesha mshambuliaji Daniel Sturridge, amefunga magoli sita kati ya mechi nane za ligi alizocheza dhidi ya Newcastle ingawa hatacheza mchezo huo huku pia Fabio Borini akifunga magoli matatu kati ya mechi tatu za ligi alizocheza dhidi ya Newcastle.
Kikosi cha Liverpool kinaweza kuwa hivi: Mignolet; Johnson, Skrtel, Lovren, Moreno; Gerrard, Henderson, Allen; Lallana, Sterling, Balotelli.
Rekodi zinaonyesha kati ya michezo 156 iliyowakutanisha Newcastle na Liverpool, Newcastle imeshinda michezo 42 huku Liverpool ikishinda michezo 75 na wametoka sare michezo 39.
0 comments:
Post a Comment