Timu ya taifa ya Hispania yaporomoka viwango vya FIFA
Na Florence George
Timu ya taifa ya Hispania imeporomoka hadi nafasi ya 11 katika viwango vya FIFA vilivyotoka leo hii na hiyo ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kuwa nje ya timu 10 za mwanzo tangu mwaka 2007.
Mabingwa hao watetezi wa Ulaya hawakufanya vizuri katika michuano ya kombe la Dunia iliyofanyika mwaka 2014 nchini Brazil na ilitolewa katika hatua ya makundi.
Timu ya taifa ya Ujerumani ambao ni mabingwa watetezi wa kombe la Dunia wameendelea kuwepo katika timu tano za juu kwa miaka minne ya hivi karibuni kwani Wanashika nafasi ya kwanza huku nafasi ya pili ikishikwa na Argentina,Colombia nafasi ya tatu,Ubeligiji ya nne na Uholanzi inakamilisha timu tano za juu.
Nayo timu ya taifa ya Uingereza imeendelea kushuka hadi nafasi ya 17 nyuma ya timu za Romania na Czech Republic,kuporomoka kwa timu hiyo kunatokana na sababu mbalimbali moja wapo ni kufanya vibaya katika kombe la Dunia lililofanyika nchini Brazil japo imefanikiwa kushinda michezo yake minne ya kufuzu kombe la EURO 2016 mpaka sasa.
Timu ya taifa ya Marekani imeshuka nafasi moja ambapo sasa inashika nafasi ya 32 huku Algeria ikiendelea kuwa timu ya kwanza kutoka barani Afrika katika timu 20 za kwanza kwa kushika nafasi ya 18.
Hizi ndio timu 10 bora katika viwango hivyo;
1.Ujerumani
2.Argentina
3.Colombia
4.Ubeligiji
5.Uholanzi
6.Brazil
7.Ureno
8.Ufaransa
9. Uruguay
10.Italia
0 comments:
Post a Comment