Searching...
Image and video hosting by TinyPic
16 November 2014
Sunday, November 16, 2014

Mwambusi bado ni kocha wa Mbeya City.




Na Oscar Oscar Jr

Kumekuwa na taarifa za kocha mkuu wa timu ya Mbeya City, Juma Mwambusi kujiondoa kwenye nafasi yake kutokana na madai mbalimbali na kubwa zaidi, ikiwa ni kutofanya vizuri kwa kikosi chake ambacho mpaka sasa kinaburuza mkia kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara.

Akiongea na kituo cha Redio cha E-fm cha jijini Dar Es Salaam jioni ya leo, katibu mkuu wa timu ya Mbeya City, bwana Emmanuel Kimbe, amekanusha taarifa za kocha huyo kuwasilisha barua ya kujiuzuru na ameongeza kuwa, bado Uongozi wa timu hiyo unamtambua kama kocha mkuu.

Kimbe ameeleza kuwa hadi jana jioni,  mwalimu huyo aliyeipandisha timu daraja na msimu uliopita akiiwezesha kumaliza kwenye nafasi ya tatu, alikuwa na mipango ya kuona ni kwa namna gani timu inaweza kurejea kwenye ubora wake pale ligi hiyo itakaporejea baada ya mapumziko.

Taarifa zimeenea tangu jana kuwa kocha huyo ameamua kujiuzuru nafasi yake kufuatia uongozi wa timu hiyo kushindwa kutimiza mahitaji yake ya kusajili wachezaji anaowataka huku wakiripotiwa pia kuto malizia fedha za usajili kwa baadhi ya wachezaji. 

Uongozi huo pia unadaiwa kuwa kwenye mgogoro wa chini kwa chini huku kila mtu akizitolea macho fedha ambazo klabu hiyo inazipata kupitia wadhamini wa klabu hiyo.

Katibu mkuu huyo ameeleza kuwa endapo kuna taarifa za kocha huyo kuondoka, labda watazipata kesho lakini mpaka sasa, wao hawana taarifa hizo na wamekuwa wakizisikia tu kwenye vyombo mbalimbali vya habari na kwenye mitandao ya kijamii.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!