Searching...
Image and video hosting by TinyPic
26 December 2014
Friday, December 26, 2014

Kuelekea: Mtibwa Sugar vs Stand United


Na Oscar Oscar Jr

Vinara wa ligi kuu Tanzania bara, timu ya Mtibwa Sugar leo hii wakiwa katika dimba la Manungu kule Turiani Mkoani Morogoro watashuka kuwakaribisha Stand United kutoka mkoani Shinyanga kwenye muendelezo wa mzunguko wa nane wa ligi kuu Tanzania bara.

Mtibwa Sugar wanaongoza ligi hiyo wakiwa na alama 15 huku wakiwa wameshafunga magoli 10 mpaka sasa. Mtibwa Sugar bado hawajapoteza hata mchezo mmoja huku safu yao ya ulinzi nayo ikionekana kuwa imara kwani mpaka sasa wameruhusu mabao natatu pekee.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime amekuwa akijivunia washambuliaji wake Ame Ally ambaye ndiye kinara wa ufungaji kwani mpaka sasa ameshafunga magoli manne huku mkongwe Mussa Hassan Mgosi naye akiwa imara na tayari amefunga kwenye mechi kidhaa ikiwamo ile iliyomkutanisha na timu yake ya zamani ya Simba.

Kwa upande wa Stand United nao wanaonekana kuimarika hasa kufuatia kusajili wachezaji kama Harouna Chanongo kwa mkopo kutoka klabu ya Simba na tayari ameonekana kufunga mabao mawili kwenye mechi za kirafiki tangu ajiunge na timu hiyo.

Stand United wanaonekana kufanya vema zaidi wanapocheza ugenini kuliko nyumbani kwani mpaka sasa, hakuna mchezo wowote waliopoteza ugenini. 

Katika kuonyesha ubora wao, waliweza kuwafunga Mgambo Shooting ugenini kabla ya kutoka sare na Simba na baadaye timu ya Kagera Sugar.

Bado safu ya ushambuliaji kwa upande wa Stand United haionekani kuwa imara kwani wamefunga mabao matano tu tangu kuanza kwa ligi kuu huku safu yao ya ulinzi ikiruhusu mabao tisa mpaka sasa. 

Stand ambao wanakamata nafasi ya 10, watashuka dimbani huku wakiwa na kumbukumbu ya matokeo ya sare kwenye mchezo wao wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Mwadui Fc ambapo mchezo huo ulimalizika kwa timu hizo kufungana bao 3-3.

Ushindi kwa Mtibwa Sugar utawafanya wazidi kujichimbia kileleni na kuziacha mbali timu za Yanga, Azam na Kagera Sugar ambazo zinapointi 13. Kagera Sugar walicheza jana uwanja wa Taifa na kuichapa Simba bao 1-0 na kujipatia ushindi wao tatu msimu huu.

Stand United ni miongoni mwa timu nne ambazo zina pointi tisa kila moja na ushindi kwenye mchezo wa leo, utaifanya timu hiyo kutimiza pointi 12 na kutinga kwenye timu saba za juu kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!