Na Chikoti Cico
Timu ya Chelsea inayoongoza ligi kuu nchini Uingereza ikiwa na alama 33 baada ya michezo 12 imetoka sare ya bila kufungana na timu ya Sunderland katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa Chelsea kutoka sare isiyo na magoli toka kuanza kwa msimu huu.
Katika mchezo huo sehemu kubwa ilitawaliwa na Chelsea ambao walimiliki mpira kwa asilimia 64 dhidi ya 36 za Sunderland huku Chelsea wakipata kona nane dhidi ya mbili za Sunderland pia Chelsea ilipiga piga mashuti 26 ambayo sita tu ndiyo yalilenga lango.
Kwa sehemu kubwa ya mchezo timu ya Sunderland “ilipaki basi” kwa kukabia chini sana kwenye eneo lao la goli huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza (counter attack) hasa kwenye dakika 10 za mwisho za mchezo huo.
Baada ya mchezo huo kocha wa Chelsea akiongea na vyombo vya habari alisema “Nafikiri wazi kabisa timu moja ilitaka kushinda, timu nyingine ilitaka kutuzuia kushinda lakini wamefanya vyema, walizuia sana na walizuia vizuri, sio kosa ni mbinu na walifanya vizuri kwa walivyocheza”
Aliendelea kusema “wachezaji wangu walijaribu kilakitu tulichoka kidogo lakini sina kitu kibaya cha kusema kuhusu wachezaji wangu, nafikiri Sunderland walizuia vizuri sana, hatukubadilisha mchezo wetu tulijaribu kila mara kucheza, tulijaribu wachezaji wapya kutupa kushambulia zaidi lakini mchezo ulikuwa mgumu kwetu”
Pamoja na sare hiyo Chelsea wameendelea kujikita kileleni mwa ligi kuu nchini Uingereza kwa kufikisha alama 33 huku pia wakiendeleza rekodi ya kutokufungwa katika mechi 20 walizocheza toka kuanza kwa msimu wa 2014/15.
0 comments:
Post a Comment