Uchambuzi; Tanzania Prisons vs Ruvu JKT.
Na Oscar Oscar Jr
Ukitazama msimamo wa ligi kuu Tanzania bara, utagundua kuwa timu za majeshi hazijaanza vema msimu huu na ni Tanzania Prisons pekee inayoonekana kufanya vizuri na kushika nafasi ya sita baada ya kushinda mchezo wake wa kwanza, kupoteza mmoja na kutoka sare dhidi ya bingwa mtetezi, timu ya Azam.
Ruvu JKT wanabaki kwenye nafasi ya 13 baada ya kupoteza michezo miwili na kutoka sare mchezo mmoja. Walianza ligi kwa kutoka sare na Mbeya City kwenye uwanja wa Sokoine ambao utatumika pia kwenye mchezo wa siku ya jumapili watakapo umana na Tanzania Prisons.
Tanzania Prisons msimu uliopita, walilazimika kusubiri ushindi kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Ashanti United ili kupata nafasi ya kubakia kwenye ligi kuu.
Ni wazi kuwa msimu huu, wasingependa kuona yanawakuta ya msimu uliopita na ndiyo maana unaona namna wanavyopambana.
Mambo si mazuri kwa upande wa Ruvu JKT na moja ya sababu kwa timu hii kutofanya vizuri msimu huu, ni kuwakosa baadhi ya nyota wake kwenye michezo ya awali ambao wamekwenda kozi ya kijeshi na kumuacha kocha Felix Minziro akiwa na kikosi finyu.
Matokeo ya Tanzania Prisons kwa michezo ya hivi karibuni.
Ruvu Shoooting 0-0 Tanzania Prisons
Yanga 2-1 Tanzania Prisons
Tanzania Prisons 0-0 Azam fc
Matokeo ya Ruvu JKT kwa michezo ya hivi karibuni.
Mbeya City 0-0 JKT Ruvu
Ruvu JKT 0-2 Kagera Sugar
Yanga 2-1 Ruvu JKT
Jabir Azizi ni moja ya wachezaji wenye uzoefu wa ligi kuu na amekuwa na mchango mkubwa tangu ajiunge na maafande wa Ruvu JKT kutoka mkoa wa Pwani.
Alifunga bao zuri sana kwenye mchezo wao na Yanga licha ya kuwa walipoteza mechi hiyo. Unapo muunganisha na washambuliaji kama Gido Simon na Reliant Lusajo, kuna uwezekano mkubwa Ruvu akafanya vizuri katika mchezo huo.
Kwa upande wa Tanzania Prisons, wanaonekana kucheza kwa jihadi kuanzia dakika ya kwanza hadi kipyenga cha mwisho na ukitazama mchezo wao dhidi ya Yanga na ule wa Azam, wamefanikiwa kuthibitisha hilo.
Kwasababu Mbeya City wanacheza siku moja kabla, ni wazi kuwa wakazi wa Mbeya watawashangilia kwa nguvu maafande hao wa Magereza.
Nani kuibuka na alama tatu? hii ni vita ya wanajeshi watupu, pengine ni vema sisi raia kazi yetu ikabaki kwenda kwenye dimba la Sokoine kule jijini Mbeya na kutazama kandanda safi.
0 comments:
Post a Comment