Uchambuzi: Ndanda fc vs Ruvu Shooting
Na Oscar Oscar Jr
Ndanda fc na Kagera Sugar ndiyo timu pekee za Ligi kuu Tanzania bara ambazo hazijaonja ladha ya kucheza kwenye dimba la nyumbani msimu huu. Timu ya Ndanda kwa mara ya kwanza watakuwa kwenye dimba la nyumbani Jumamosi hii dhidi ya timu ya Ruvu Shooting kutoka mkoa wa Pwani.
Mpaka mzunguko wa tatu unakamilika, Ndanda ndiyo timu pekee iliyofunga magoli mengi kwenye mchezo mmoja. Ilifanya hivyo pale ilipoitandika Stand United ugenini kwenye dimba la Kambarage bao 4-1 wakati timu hizo zote zikiwa ndiyo zimepanda daraja msimu huu kucheza ligi kuu.
Ruvu Shooting ndiyo timu inayoburuza mkia mpaka sasa ikiwa nafasi ya 14 baada ya kutoka sare mchezo mmoja na kupoteza michezo yake mingine miwili. Ndanda wanashika nafasi ya tisa huku wakiwa na alama tatu pekee baada ya mzunguko wa tatu kamalizika.
Matokeo ya Ndanda Fc kwa mechi za hivi karibuni.
Stand United 1-4 Ndanda fc
Mtibwa Sugar 3-1 Ndanda fc
Coastal Union 2-1 Ndanda fc
Matokeo ya Ruvu Shooting kwa mechi za hivi karibuni.
Ruvu Shoooting 0-2 Tanzania Prisons
Azam fc 2-0 Ruvu Shooting
Ruvu Shooting 0-0 Mbeya City
Mchezaji wa kuchungwa kwa upande wa Ndanda fc
Jacob Massawe ni moja ya washambuliaji wa Ndanda wenye ubora na uzoefu wa ligi kuu. Alifanya vizuri sana kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Simba na hata ule wa fungua dimba dhidi ya Stand United. Bado hajafunga goli lolote lakini ni mzuri pia katika kutengeneza nafasi kwa wachezaji wenzie.
Mchezaji wa kuchungwa kwa upande wa Ruvu Shooting.
Juma Nade ni mshambuliaji ambaye ana uwezo mkubwa wa kupiga mipira ya mbali na kama walinzi wa Ndanda watampa nafasi ya kufanya hivyo, anaweza kuwapatia Ruvu Shooting bao lao la kwanza la msimu. Alicheza dhidi ya Azam lakini Ulinzi bora wa Agrey Moris na wenzake, ulifanya akose jipya na kocha akampumzisha kipindi cha pili.
Jacob Massawe na Hamis Salehe, wote msimu uliopita walikuwa na kikosi cha JKT Oljoro na kwa sasa wanatengeneza safu ya ushambuliaji ya Ndanda.
Ni wazi kuwa Ruvu Shooting watakuwa kwenye wakati mgumu mbele ya wanamtwara. Nani ataibuka kidedea? Tukutane kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona siku ya Jumamosi.
0 comments:
Post a Comment