Na Oscar Oscar Jr
Mechi nyingine itakayo zikutanisha timu zinazotoka mji mmoja, itapigwa pale kwenye dimba la Mkwakwani jijini Tanga ambapo Mgambo JKT watawakaribisha Coastal Union kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara siku ya jumamosi.
Coastal Union wako kwenye nafasi ya saba baada ya kujikusanyia alama nne kutokana na michezo mitatu ya ligi kuu. Coastal Union watakuwa wanarejea tena kwenye dimba la Mkwakwani baada ya kucheza hapo mechi yao iliyopita dhidi ya Ndanda fc baada ya michezo yao ya awali kucheza ugenini Dar es salaam dhidi ya Simba na Mbeya dhidi ya Mbeya City.
Nao Mgambo JKT wako kwenye nafasi ya 11 baada ya kuanza ligi kwa ushindi dhidi ya Kagera Sugar kabla ya kufanya vibaya dhidi ya Stand United na Mtibwa ya Morogoro. Kocha wa Mgambo aliwahi kufanya kazi na benchi la ufundi la Coastal Union na tayari ameanza tambo kuwa atawafunga Coastal Union.
Msimu wa 2012/2013 timu hizi zilikutana na mechi zote mbili, Mgambo JKT walifungwa. Mechi ya kwanza Coastal walishinda 1-0 na mchezo wa marejeano, ulimalizika kwa Coastal Union kushinda magoli 3-1. Hali ilikuwa tofauti msimu uliopita ambapo mechi ya kwanza ilikwisha kwa sare tasa huku mchezo wa marejeano, Mgambo akiibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Mechi tatu za Coastal Union za msimu huu.
Simba 2-2 Coastal Union
Mbeya City 1-0 Coastal Union
Coastal Union 2-1 Ndanda fc
Mechi tatu za Mgambo JKT msimu huu
Mgambo JTK 1-0 Kagera Sugar
Mgambo JKT 0-1 Stand United
Mtibwa Sugar 1-0 Mgambo JKT
Mchezaji wa kuchungwa kwa Coastal Union
Pamoja na kuwa timu ya Coastal Union imefunga mabao manne mpaka sasa, Rama Salim, Yayo Lutimba, Joseph Mahundi na Hussein Swed ndiyo wafungaji, bado namtazama Yayo Lutimba kama mchezaji anayeweza kuisaidia Coastal Union kwenye mchezo huo kutokana na umahiri wake dimbani.
Mchezaji wa kuchungwa kwa Mgambo JKT
Baada ya kufunga bao moja dhidi ya Kagera Sugar, Ramadhani Pera anaweza kudhihirisha ubora wake tena kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union. Bado Mgambo inaonekana sio timu nzuri hasa kwenye safu ya ushambuliaji na ndiyo maana unaweza kushuudia mechi hiyo magoli yakafungwa na walinzi au viungo wa kati.
Pamoja na kuonyesha matumaini makubwa msimu huu, timu ya Coastal Union bado ina mivutano ya ndani kwa ndani baina ya viongozi wa klabu hiyo na wanachama.
Kama ilivyo kwa timu nyingi za wananchi, mivutano hii ikizidi inaweza kuharibu mwenendo wa timu kiwanjani. Nani atapoteza mchezo huo? Tukutane Mkwakwani siku ya Jumamosi.
0 comments:
Post a Comment