Valencia vs Real Madrid: Leo saa 1:00 Usiku
Na Oscar Oscar Jr
Huu utakuwa mwezi mgumu sana kwa Real Madrid kufuatia kuwa na mechi 10 ndani ya siku 32 huku baadhi ya mechi hizi zikiamua kuwepo au kuendolewa kwenye mataji ambayo wanashiriki msimu huu. Leo majira ya saa 1:00 Jioni watakuwa ugenini kwenye dimba la Mestalla kucheza na timu ngumu ya Valencia.
Real Madrid watashuka dimbani leo hii kutaka pointi tatu muhimu huku wakifahamu kuwa, matokeo tofauti na ushindi yatawapa mwanya Barcelona ambao wanashika nafasi ya pili kuweza kushika usukani wa ligi hiyo endapo wataibuka na ushindi kwenye mchezo wao wa leo utakaopigwa ugenini Anoeta dhidi ya Real Sociedad.
Kuelekea mchezo huo, kocha Carlo Ancelotti amesema atatumia kikosi cha kwanza na wala hafikirii mchezo unaofuata wa kombe la Mfalme utakaowakutanisha na watani zao wa jadi, Atletico Madrid.
Valencia ni moja kati ya timu ngumu msimu huu kwenye La Liga na mpaka sasa wameshashinda mechi tisa na kujikusanyia alama 31 zilizowafikisha nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu.
Bila shaka Real Madrid ambao hawajapoteza mchezo wowote kwenye mechi 22 za kiushindani za hivi karibuni, watakuwa na kiu ya kuendeleza ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa ambao msimu uliopita ulichukuliwa na majirani zao Atletico Madrid.
Safu ya ushambuliaji ya Real Madrid tayari imeshafunga mabao 45 huku Christiano Ronaldo akiwa na mabao 25 na leo atataka kuongeza wigo kati yake na Lionel Messi ambaye anamfuatia akiwa na mabao 15.
Huu ni mtihani mwingine kwa safu ya ulinzi ya Valencia kumzuia Ronaldo mwenye magoli 25, Benzema mwenye magoli nane na Bale ambaye ameshafunga mara saba msimu huu.
0 comments:
Post a Comment