Searching...
Image and video hosting by TinyPic
24 October 2014
Friday, October 24, 2014

NIFIKIRIAVYO: Liverpool wanapomgeuza Balotelli Jalala.


Na Chikoti Cico


Katika moja ya mambo marahisi duniani kwa mwanadamu yeyote hasa mambo yanapoenda mrama ni kulaumu watu wengine.

kwenye familia watoto wanawalaumu wazazi kwa kushindwa kutafuta mali za kutosha kuwawezesha wao kuishi vizuri na wazazi nao, wanawalaumu watoto kushindwa kusoma kwa bidii mpaka maisha yakawa magumu kwao.

Ukirudi kwa wananchi ni kuilaumu serikali, hata katika mambo ambayo yangewezekana kufanyika bila mkono wa serikali bado watu watailaumu serikali na upande wa pili, serikalini wanageuza kibao na kuwalalamikia wananchi ilimradi kila mtu anatafuta mtu wa kumlaumu ili kujiridhisha nafsi yake.

Tangu klabu ya Liverpool ilipomuuza mshambuliaji Luis Suarez mapema mwezi wa saba mwaka huu, mpaka sasa timu ya Liverpool haijakaa sawa ukifananisha na msimu wa ligi uliopita ambao walimaliza nafasi ya pili na kupata nafasi ya kurejea kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya.

Baada ya kumuuza Suarez kwa timu ya Barcelona kwa kiasi cha paundi milioni 75 kocha Brendan Rodgers, akatumia zaidi ya paundi milioni 100 kufanya usajili wa wachezaji nane akiwemo mshambulaiji Mario Balotelli aliyenunuliwa toka AC Milan kwa kiasi cha paundi milioni 16 kuja kuziba pengo la Suarez.

 Mpaka sasa, Balotelli ameshindwa kuonyesha makali yake huku akifunga goli moja tu kati ya michezo 10 ambazo ameichezea Liverpool msimu huu.

Kushindwa huko kwa Mario Balotelli kuziba pengo la Suarez hasa baada ya mshambuliaji mwingine wa Liverpool Daniel Sturridge kuumia, kumekuwa ni chanzo cha lawama kwa kila matokeo mabovu ambayo Liverpool amekuwa akiyapata kwenye ligi kuu ya Uingereza na ligi ya mabingwa Ulaya.

Mpaka sasa Liverpool inashika nafasi ya tano ikiwa na alama 13 kwenye msimamo wa ligi kuu ya Uingereza huku pia ikishika nafasi ya tatu ikiwa na alama tatu kwenye msimamo wa kundi B wa ligi ya Mabingwa Ulaya.

 katika michuano hiyo yote miwili, Liverpool wamekuwa wakisua sua ukiuliza ni kwanini? majibu ni maneno mawili tu “Mario Balotelli” bila kuangalia sababu zingine.

Usajili wa Balotelli ulienda sambamba na usajili wa Lambert, Emre, Moreno, Markovic, Lallana, Levron na Origi(yuko kwa mkopo Lille) katika wote hao waliosajiliwa hakuna anayeandamwa kwamba anacheza chini ya kiwango zaidi ya Balotelli.

 Hakuna mchambuzi anayeongea kuhusu Brendan kutumia paundi zaidi ya milioni 100 kwenye usajili lakini bado timu inakosa kuonyesha kiwango kizuri. 

Labda inawezekana usajili ni kama kamari kwamba unaweza ukamsajili mchezaji na akaonyesha kiwango kizuri ama ashindwe kucheza vyema.

lakini swali la kujiuliza ni kwamba wakati Brendan anamsajili Balotelli kwa paundi milioni 16 sokoni, kulikuwa na washambuliaji bora zaidi yake kama Falcao, Costa, Cavani ambao labda wanafikia kiwango cha Suarez lakini wote hao aliwaacha vipi leo ajifiche nyuma ya ubovu wa Balotelli?

Mpaka sasa Brendan amekuwa akijificha nyuma ya kiwango kibovu cha Balotelli kila Liverpool inapopata matokeo mabovu.

Mechi dhidi ya Real Madrid jambo lililozungumziwa sana na Brendan, mashabiki wa Liverpool na wachambuzi wa soka duniani, ni kitendo cha Balotelli kubadilishana jezi na Pepe wakati wa mapumziko, wakiacha kuzungumzia ubovu wa beki ya Liverpool ambayo mpaka sasa imeruhusu jumla ya magoli 17.

Pamoja na Balotelli kuonyesha kiwango kibovu kati ya mechi 10 alizoichezea Liverpool ni vyema akapewa nafasi zaidi na sio kugeuzwa jalala kwa kila baya linalotokea pale Anfield hata kwa makosa ambayo yanamuhusu moja kwa moja kocha mkuu wa Liverpool.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!