Searching...
Image and video hosting by TinyPic
6 April 2014
Sunday, April 06, 2014

YANGA YAMPIGA RUVU JKT MKONO WA NYANI!



Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara timu ya Young fricans leo imeibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya timu ya Maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini JKT Ruvu katika mchezo uliofanyika kwenye dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Kwa matokeo ya leo kupata pointi 3, Young Africans imefikisha jumla ya pointi 49 ikiwa katika nafasi ya pili nyuma ya Azam FC yenye pointi 53 huku timu zote zikiwa zimecheza michezo sawa 23 na kubakisha michezo mitatu mitatu kabla ya kumalizika kwa Ligi Kuu.

Mrisho Ngasa aliipatia Young Africans bao la kwanza dakika ya 8 ya mchezo baada ya kuitumia vizuri pasi ya mshambuliaji Didier Kavumbagu aliyewatoka walinzi wa JKT Ruvu na kumpasia mfungaji ambaye hakufanya makosa katika umaliziaji.

Dakika ya 15 ya mchezo, Mrisho Ngasa aliipatia Young Africans bao la pili baada mshambuliaji wa pembeni Saimon Msuva kuwatoka walinzi wa JKT Ruvu na kumimina krosi iliyomkuta Ngasa amabye nae bila ajizi aliukwamisha mpira wavuni.

Didier Kavumbagu ambaye alikuwa mwiba mkali kwa walinzi wa JKT Ruvu aliipatia Young Africans bao la tatu la mchezo baada kutengenezewa pasi mpenyezo na Mrisho Ngasa aliyewatoka walinzi na viungo wa JKT Ruvu.

Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Young Africans 3 - 0 JKT Ruvu.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko, Hussein Javu aliingia kuchukua nafasi ya Hamis Kiiza aliyeumi aliongeza kasi ya mashambulizi na kuifanya safu ya ulinzi  ya JKT kuwa kwenye wakati mgumu wakati wote wa mchezo.

Dakika ya 49 Mrisho Ngasa aliwainua tena vitini wapenzi, washabiki na wanachama wa Young Africans baada ya kuipatia timu yake bao la nne kufuatia pasi ya Saimon Msuva aliyemtoka mlinzi wa Omar Mtaki wa Ruvu JKT.

Hussein Javu alihitimisha karamu ya ushindi kwa Young Africans dakika ya 52 ya mchezo baada ya kuipatia timu yake bao la tano kufuatia kuwatoka walinzi wa JKT Ruvu kuanzia eneo la mitaa 35 na kuwakimbiza mpaka kumchambua mlinda mlango Shaban Dihile.

JKT Ruvu walijipatia bao la kufutia machozi dakika ya 84 ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji wake Idd Mbaga kwa kichwa baada ya krosi ya Damas Makwaya kuwapita walinzi wa Young Africans na kumkuta mfungaji.

Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika Young Africans 5 - 1 JKT Ruvu.
Young Africans: 1. Deo Munish "Dida" 2.Juma Abdul, 3.Oscar Joshua, 4.Nadir Haroub "Cannavaro". 5.Mbuyu Twite, 6.Frank Domayo, 7.Saimon Msuva, 8.Hassan Dilunga/Hamis Thabit, 9.Didier Kavumbagu/Jerson Tegete, 10.Mrisho Ngasa, 11.Hamisi Kizza/Hussein Javu

Taarifa hii ni kwa mujibu wa website ya YANGA

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!