IVORY COAST wamepagawa. Dakika chache kabla hawajapanda ndege na
kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar
es Salaam juzi Alhamisi usiku, mastaa wawili wa timu hiyo, Jean-Jacques
Gosso Gosso na kinda wa Manchester City, Abdul Razak wametiana ngumi
uwanja wa mazoezi na mmojawapo ametimuliwa.
Ivory Coast itacheza na Taifa Stars kesho Jumapili katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 9:00 alasiri.
Bila ya kujua chanzo cha ugomvi huo katika Uwanja
wa Felix Houphouet Boigny, Gosso Gosso anayekipiga katika klabu ya
Mersin Idmanyurdu ya Uturuki alionekana akiwa amemkaba kabali Razak
ambaye inasemekana ndiye chanzo cha ugomvi huo.
Kiungo Yaya Toure ambaye alilikosa pambano
lililopita dhidi ya Taifa Stars Juni mwaka jana nchini Ivory Coast
alionekana kupumbazwa na ugomvi huo uliotokea karibu yake ambao
ulimuhusu kinda wao wa Manchester City ambayo imekuwa ikikumbwa na
kashfa ya ugomvi wa mazoezini mara kwa mara.
Kutokana na ugomvi huo,Razak ameondolewa katika
kambi ya Ivory Coast na hakusafiri na wenzake katika kikosi kilichotua
Dar es Salaam kwa ndege ya kukodi.
Kwa Toure, hilo linaendelea kuwa tukio jingine mbele ya macho yake linalomuhusu mchezaji wa Manchester City.
Katika uwanja wa mazoezi wa klabu yake kwa nyakati
tofauti amewahi kuwashuhudia mastaa wa Man City kama vile, Mario
Balotelli, Jerome Boateng, Micah Richards na hata kocha wa zamani,
Roberto Mancini wakijihusisha na ugomvi.
0 comments:
Post a Comment