KWA maneno rahisi sana ni hivi; Taifa Stars ikipata sare au
kupoteza mchezo wa kesho Jumapili dhidi ya Ivory Coast biashara yetu
itakuwa imekwisha.
Lakini, haiwezekani hawa Ivory Coast waliopigana mazoezini watuletee jeuri, tena nyumbani kwetu.
Watanzania tupo milioni 45, lakini ni watu 60,000
pekee ndio wataingia kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Yaani
tuzidiwe ujanja na kikundi cha watu 80 kilichokuja kutoka Ivory Coast!
Stars imeunganisha nguvu ya nchi nzima kuhakikisha
inashinda mechi zake zote mbili zilizosalia kwa kuanzia na hii ya Ivory
Coast kwenye Uwanja wa Taifa huku ikiombea angalau Morocco itoke sare
na Ivory Coast kwenye mechi ya mwisho.
Kama hesabu za Stars zikienda sawa, Stars ikaenda
na Gambia Septemba 6 ikachukua pointi tatu itaongoza Kundi C na kuingia
kwenye hatua nyingine itakayohusisha vinara kumi wa makundi yote ya
Afrika ambako kutachezwa mechi mbili za mtoano nyumbani na ugenini
kupata timu tano za kucheza Kombe la Dunia.
Kocha wa Stars, Kim Poulsen ana imani kubwa na
kikosi chake na kupoteza mabao 2-1 kwenye mechi iliyopita nchini Morocco
hakujamkatisha tamaa ndio maana amewaomba Watanzania wamuunge mkono na
kujazana uwanjani kushangilia kwa nguvu mwanzo mwisho.
“Tunacheza na timu ngumu na bora kwa bara la
Afrika. Lakini hatupaswi kuwaogopa ingawa tunatakiwa kucheza kwa
uangalifu mkubwa kwa kushambulia pamoja na kujilinda kikamilifu,
tusiachie upenyo hata kidogo wala kupepesuka kimaamuzi,” alisisitiza
kocha huyo anayeamini katika soka la vijana.
Kim alieleza kuwa wanatakiwa kuwa makini zaidi
katika dakika za mwanzo kwani iwapo wataruhusu bao la mapema linaweza
kuwachanganya vijana wake na kuwatoa mchezoni na kuongeza kuwa
kukosekana kwa wachezaji watatu; beki Aggrey Morris aliyelimwa kadi
nyekundu mechi ya Morocco, Mrisho Ngassa anayemiliki kadi mbili za njano
pamoja na John Bocco aliye majeruhi hakuwezi kuathiri timu wala
mashabiki wasihofu chochote kwani atabadili staili ya mchezo.
Katika mazoezi ya Stars, Kim amesisitiza matumizi
ya mipira ya kona pamoja na faulo kwenye kufunga na amempa Mwinyi
Kazimoto jukumu la kupiga mipira hiyo na kuwataka mabeki Nadir Haroub
Cannavaro na Erasto Nyoni kuhakikisha wanatumia vizuri uzoefu wao
kufunga mipira ya vichwa.
WACHEZAJI
Nahodha wa Stars na kipa mwenye heshima kubwa
nchini, Juma Kaseja alisema; “Tumejifua vya kutosha, mchezo hautakuwa
rahisi kwetu. Ivory Coast ni timu bora Afrika, ina wachezaji wengi
wanaocheza soka Ulaya, mashabiki watusapoti tufanye kazi kwa vitendo.
Tupo vizuri na mwalimu ametupa mbinu nyingi. Tunawaahidi tutapambana
hadi tone la mwisho kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.”
Kiraka Shomari Kapombe alisema: “Nafikiri tupo
sawa kimwili na kiakili. Mwalimu ametupa mbinu nyingi namna ya
kuwamaliza Ivory Coast katika mazoezi. Nadhani kilichobaki ni kuzifanyia
kazi, mashabiki wajitokeze kwa wingi, waje kufurahi. Tunawaahidi kuwa
tutacheza vizuri pamoja na kuwapa furaha ya ushindi.”
0 comments:
Post a Comment