Searching...
Image and video hosting by TinyPic
21 November 2014
Friday, November 21, 2014

Uchambuzi: Arsenal vs Manchester United



Na Chikoti Cico

Ligi kuu nchini Uingereza inatarajiwa kuendelea tena wikendi hii na moja ya mechi inayosuburiwa kwa hamu na wapenzi wengi wa soka duniani ni kati ya Arsenal dhidi ya Manchester United, mchezo utakaopigwa kwenye uwanja wa Emirates jijini London majira ya saa 2:30 Usiku.

Timu ya Arsenal inayofundishwa na kocha Arsene Wenger, itaingia kwenye mchezo huo huku ikiendelea kuwakosa Laurent Koscielny, Mesut Ozil, Mathieu Debuchy, David Ospina na Abou Diaby ambao ni majeruhi

Kurejea kwa mshambuliaji Olivier Giroud na kiungo Mikel Arteta kunatarajiwa kuiongezea Arsenal nguvu kuelekea kwenye mchezo huo.

Arsenal maarufu kama washika bunduki wa jiji la London, mpaka sasa wanashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 17 huku wakiwa wameshinda michezo minne na kutoka sare michezo mitano na kupoteza michezo miwili na hivyo kupitwa kwa alama 12 na Chelsea wanaongoza ligi hiyo.

Kocha Wenger anatarajia kuingia kwenye mchezo huo kutafuta ushindi wa tatu nyumbani huku akimtegemea zaidi mshambuliaji wake Alex Sanchez kuongoza safu ya ushambuliaji ya Arsenal, mpaka sasa Sanchez ameshaifungia Arsenal magoli 12 katika michezo 14 ya mashindano mbalimbali aliyocheza.

Kikosi cha Kocha Wenger kinaweza kuwa hivi: Szczesny; Chambers, Mertesacker, Monreal, Gibbs; Flamini, Ramsey; Cazorla, Wilshere, Sanchez; Welbeck

Kwa upande wa Manchester United, nao wanasumbuliwa na wachezaji wengi walioko majeruhi na katika mchezo huo wanatarajiwa kuwakosa mshambuliaji Radamel Falcao mabeki Marcos Rojo, Phil Jones, Jonny Evans, Rafael na kiungo Daley Blind ambao ni majeruhi huku beki wa kushoto Luke Shaw akiwa na hatihati ya kutokucheza mchezo huo

Kocha wa Manchester United, Mdachi Luis Van Gaal anatarajia kuingia kwenye mchezo huo kutafuta ushindi wa kwanza ugenini kwani mpaka sasa United wameshinda michezo minne ambayo yote wameshindia nyumbani Old Trafford huku wakishika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 16, alama moja chini ya Arsenal.

Takwimu zinaonyesha katika michezo 14 iliyopita waliyokutana Arsenal na Manchester United katika mashindano mbalimbali United wameweza kushinda michezo 10, kutoka sare mchezo mmoja na Arsenal kushinda mchezo mmoja.

Nahodha wa United, Wayne Rooney anashikilia rekodi pamoja na Robbie Fowler kwa kuongoza kuifunga Arsenal kuliko wachezaji wengine kwenye historia ya ligi ya Uingereza huku wote wakifunga kila mmoja magoli 10.

Kikosi cha kocha Van Gaal kinaweza kuwa hivi: De Gea; Valencia, Smalling, Blackett, Shaw; Fellaini, Herrera; Januzaj, Rooney, Mata, Van Persie

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!