UONGOZI wa Halmashauri ya Mbeya, umembakiza kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi katika ajira yake baada ya kufikia makubaliano katika vikao vyao vilivyokuwa vikifanyika kwa wiki nzima.
Mwambusi aliandika barua ya kujiuzulu kufundisha
timu hiyo ambayo imefanya vibaya katika mechi zake saba na kushika
nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi tano
pekee ikifungwa mechi nne mfululizo, ikishinda moja na kutoka sare mechi
mbili.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo, zilisema kwamba
tayari Mwambusi amekubali kuendelea kuifundisha timu hiyo ambayo msimu
uliopita ilishika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na
kuacha gumzo katika ligi hiyo.
“Mwambusi amekubaliana na viongozi wake kuendelea
kuifundisha timu, kwa kipindi hiki isingekuwa rahisi kupata kocha
mwingine kwani ni mapumziko ya muda mfupi, hivyo wamemwomba aendelee na
ajira yake ikiwemo kurekebisha baadhi ya mambo ambayo kocha huyo ametaka
yafanyike,” kilisema chanzo hicho.
Akitoa ufafanuzi huo, Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema: “Mwambusi ni kocha wetu na ni mfanyakazi wetu lakini kila kitu kitajulikana zaidi kesho (leo) Jumatatu, kwani kwa sasa siwezi kuzungumza zaidi juu ya hilo mpaka kesho.”
Source: Gazeti la Mwanaspoti la leo
0 comments:
Post a Comment