Na Chikoti Cico
Nahodha wa timu ya Manchester City ya Uingereza, Vicent Kompany anatarajiwa kurejea uwanjani kuichezea timu hiyo baada ya kuwa nje kwa muda kutokana na kuumia kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya CSKA Moscow wiki mbili zilizopita.
Kompany aliyekosa mechi iliyopita ya ligi dhidi ya QPR mchezo ulioisha kwa Manchester City kutoa sare ya magoli 2-2, anatarajiwa kucheza dhidi ya Swansea City siku ya Jumamosi katika mfululizo wa mechi za ligi kuu nchini Uingereza hasa baada ya kuonekana akiendelea vizuri katika mazoezi ya kujiandaa na mchezo huo wiki hii.
Beki huyo mahiri wa Manchester City pia alikosa mchezo wa timu yake ya taifa ya Ubelgiji dhidi ya Wales, uliopigwa Jumapili katika moja ya mechi za kufuzu kwa michuano ya EURO 2016 mchezo ulioisha kwa sare ya bila kufungana.
Kurejea kwa Kompany kutakiongezea makali kikosi cha kocha wa Manchester City, Manuel Pellegrini kwenye sehemu ya ulinzi katika maandalizi ya mechi za ligi ya Uingereza lakini pia, maandalizi mechi za ligi ya mabingwa Ulaya hasa kwenye mchezo dhidi ya Bayern Munich ambao City wanahitajika kushinda ili kufufua matumaini ya kuvuka hatua ya makundi ya mchuano hiyo.
Pamoja na kurejea kwa Kompany, timu ya Manchester City ambayo inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 21 bado itaendela kuwakosa kiungo David Silva, beki Aleksandar Kolarov na mshambulaji Edin Dzeko katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Swansea.
0 comments:
Post a Comment