Na Chikoti Cico
Mshambuliaji wa timu ya Arsenal kutoka Ufaransa, Olivier Giroud anatarajiwa kurejea uwanjani kuvaana na timu ya Manchester United katika mchezo wa kusisimua wa ligi kuu nchini Uingereza utakaopigwa siku ya Jumamosi uwanjani Emirates.
Giroud ambaye amekuwa nje toka mwishoni mwa mwezi wa nane baada ya kuvunjika kidole cha mguu kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Everton ulioisha kwa sare ya magoli 2-2, anatarajiwa kuwa fiti hivyo kuiongezea makali safu ya ushambuliaji ya Arsenal ambayo imekuwa ikiongozwa na Alex Sanchez wakati ambao Giroud alipokuwa nje.
Mshambuliaji huyo amepona mapema zaidi tofauti na ilivyotarajiwa kwani taarifa za awali baada ya kufanyiwa vipimo zilionyesha angeweza kurejea uwanjani mapema mwakani hivyo kurejea huko mapema kutakiongezea nguvu kikosi cha kocha wa Arsenal, Arsene Wenger hasa baada ya kuandamwa na wachezaji wengi majeruhi kwa siku za hivi karibuni.
Arsenal ambao wanashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 17 wataendelea kuwakosa mabeki Laurent Koscielny na Mathieu Debuchy huku kiungo Mesut Ozil naye akiendelea kuuguza majeraha na anatarajiwa kurejea uwanjani mapema mwaka 2015. Kurejea pia kwa kiungo Mikel Arteta ambaye alikuwa majeruhi, kutaiongezea nguvu safu ya kiungo ya Kocha Wenger.
Arsenal ambao walifungwa kwa magoli 2-1 kwenye mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Swansea City, wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo dhidi ya Manchester United hapo Jumamosi kutafuta ushindi wa hali na mali ili kupunguza tofauti ya alama 12 dhidi ya vinara Chelsea ambao wanaongoza ligi wakiwa na alama 29 lakini pia kutafuta kuingia kati ya nafasi nne za juu (top four) kwenye msimamo wa ligi hiyo.
0 comments:
Post a Comment