Searching...
Image and video hosting by TinyPic
28 June 2013
Friday, June 28, 2013

WACHEZAJI MAKINDA WAWILI WA TANZANIA WAENDA KUJIFUNZA SOKA QATAR KWENYE ACADEMY YA KIMATAIFA YA ASPIRE


Wachezaji wawili kutoka Tanzania wamechaguliwa miongoni mwa 50 waliofanyiwa majaribio nchini Uganda kwa ajili ya kuingia katika kituo cha kuendeleza vipaji (centre of excellence) kilichoko Doha nchini Qatar kupitia mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football Dream.
Abdulrasul Tahir Bitebo (15) ambaye ni mshambuliaji kutoka Kituo cha Uwanja wa Karume, na Martin Omela Tangazi (14) ambaye ni beki kutoka Kituo cha Ukonga ndiyo waliochaguliwa kutoka Tanzania kuingia katika kituo ambapo watakaa kwa mwezi mmoja kabla ya kusaini mkataba rasmi wa kuendelezwa.

Wachezaji wengine walikuwa wakitoka katika nchi za Uganda na Kenya. Mchezaji mwingine aliyefuzu katika nafasi tatu zilizokuwepo ni kutoka nchini Kenya.

Mpango wa Aspire Football Dream unafadhiliwa na Mtoto wa Mfalme wa Qatar katika nchi 16 duniani, na kwa hapa nchini uko chini ya Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

TFF ina jumla ya vituo 14 vya kuendeleza vipaji kupitia mpango huo wa Aspire Football Dream. Vituo hivyo ni Karume, Kigamboni, Tandika, Kawe, Ukonga, Kitunda, Mbagala, Magomeni, Makongo, na Tabata vilivyo katika Mkoa wa Dar es Salaam. Vingine ni Bagamoyo kilichopo mkoani Pwani, Morogoro, Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kituo kingine cha kuendeleza vipaji (centre of excellence) cha Aspire kipo Dakar nchini Senegal.

TFF KUENDESHA KOZI SITA KATI YA JULAI- SEPTEMBA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litaendesha kozi sita tofauti za mpira wa miguu kati ya Julai na Septemba mwaka huu.

Kozi hizo ni FIFA 11 For Health itakayofanyika Hombolo mkoani Dodoma kuanzia Julai 8 hadi 19 mwaka huu. Julai 6 hadi 15 mwaka huu kutakuwa na kozi ya mpira wa miguu wa ufukweni (Beach Soccer) itakayofanyika jijini Dar es Salaam.

Waamuzi wa FIFA nao watakuwa na kozi itakayofanyika kati ya Agosti 22 hadi 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati kozi ya ukocha kwa ajili ya Copa Coca-Cola itafanyika jijini Dar es Salaam kati ya Agosti 12 na 17 mwaka huu.

Vilevile kutakuwa na kozi ya mpango wa grassroots unaolenga wachezaji mpira wa miguu (wasichana na wavulana) wenye umri kuanzia miaka 6-12 itafanyika kuanzia Septemba 9 hadi 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati tamasha (festival) la grassroots litafanyika Uwanja wa Karume, Septemba 14 mwaka huu.

RCL KUKAMILISHA HATUA YA NNE JUMAPILI
Mechi za marudiano za hatua ya nne ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) zitachezwa Jumapili (Juni 30 mwaka huu) kwenye viwanja vya Sokoine jijini Mbeya, na Kambarage mjini Shinyanga.

Friends Rangers ya Dar es Salaam ambayo katika mechi ya kwanza ilifungwa nyumbani mabao 3-0 itakuwa mgeni wa Stand United FC mjini Shinyanga wakati Kimondo SC itaikaribisha Polisi Jamii ya Mara jijini Mbeya. Katika mechi ya kwanza timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.

Hatua ya mwisho ya RCL itachezwa Julai 3 mwaka huu kwa mechi za kwanza wakati zile za marudiano zitafanyika Julai 7 mwaka huu. Timu tatu za kwanza zitapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!