Searching...
Image and video hosting by TinyPic
2 December 2014
Tuesday, December 02, 2014

Uchambuzi: Arsenal vs Southampton


Na Chikoti Cico

Timu ya Arsenal kutoka London inatarajia kucheza na Southampton siku ya Jumatano kwenye uwanja wa Emirates katika mfululizo wa mechi za ligi kuu nchini Uingereza, huu ukiwa mchezo wa 14 toka kuanza kwa ligi hiyo mapema mwezi wa nane.

Kuelekea kwenye mchezo huo dhidi ya Southampton, timu ya Arsenal bado inakabiliwa na wachezaji wengi majeruhi ambao ni kipa Wojciech Szczesny, Mikel Arteta, Theo Walcott, Mesut Ozil, Mathieu Debuchy, David Ospina na Wilshere.

Vile vile kumekuwa na taarifa za kuumia kwa mabeki Nacho Monreal, Kieran Gibbs na kiungo Alex Oxlade-Chamberlain ambao wana hatihati ya kutokucheza mchezo huo siku ya Jumatano.

Mpaka sasa Arsenal inayofundishwa na kocha Arsene Wenger inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 20 baada ya kushinda mchezo uliopita dhidi ya West Bromwich kwa goli 1-0, goli lilifungwa na mshambulaiji Danny Welbeck.

Takwimu zinaonyesha Arsenal wamekuwa na rekodi nzuri kwenye ligi dhidi ya Southampton ndani ya uwanja wa Emirates kwani katika michezo 19 iliyopita ya ligi waliyocheza nyumbani dhidi ya Southampton wameshinda michezo 14 na kutoka sare michezo mitano huku wakiwa hawajafungwa mchezo hata mmoja.

Kikosi cha kocha Wenger kinaweza kuwa hivi: Martinez, Chambers, Mertesacker, Koscielny, Monreal, Flamini, Ramsey, Welbeck, Sanchez, Cazorla, Giroud

Kwa upande wa Southampton baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Manchester City kwa kufungwa magoli 3-0 wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo kwa nguvu zote wakitafuta alama tatu muhimu ili kuendelea kujikita kati ya timu nne za juu (top four) kwenye msimamo wa ligi kuu.

Mpaka sasa timu hiyo inashika nafasi ya tatu huku wakijikusanyia alama 26 baada ya kucheza michezo 13.

Kuelekea mchezo huo dhidi ya Arsenal Kocha wa Southampton Mdachi Ronald Koeman atamkosa kiungo wake mahiri Morgan Schneiderlin aliyeumia kwenye mchezo dhidi ya Manchester City hivyo nafasi yake inaweza kuzibwa na Shane Long.

Huku wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuifunga Arsenal kwenye kombe la Capital One ndani ya uwanja wa Emirates, Southampton watamtegemea zaidi mshambuliaji wao Graziano Pelle kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo katika kutafuta alama tatu muhimu mbele ya mashabiki wa Arsenal.

Kikosi cha Kocha Koeman kinaweza kuwa hivi: Forster; Clyne, Fonte, Yoshida, Bertrand; Wanyama, Alderweireld, Tadic; Long, Mane, Pelle

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!