Searching...
Image and video hosting by TinyPic
9 April 2015
Thursday, April 09, 2015

Ni wakati wa Yanga sasa kuwaangalia Waarabu kwa fikra tofauti


Na George Mganga 0688665508
Kabla ya yote kwanza nianze kutoa pole kwa ndugu yetu mchezaji Jonas Mkude kwa kufiwa na baba yake mzazi pia kwa ujumla wa wapenzi na mashabiki wote wa Simba Sports walioguswa na msiba halikadhalika kwa sisi wote wapenda soka na Taifa kwa ujumla.

Sitopenda kuwasahau ndugu zetu wanamichezo Simba UKAWA kwa ajali waliyoipata na kupelekea kupoteza maisha takribani watu 7 huko Morogoro.
Baada ya hayo napenda kuchukua fursa hii kuipongeza sana kilabu ya Yanga kwa juhudi kubwa na jitihada ilizozitumia toka huku chini na kufika hapo ilipo hadi sasa, ni hata moja nzuri na ya kuigwa hasa pale mtu au kiongozi anapofanya mazuri hana budi kuigwa na umma au raia wengine wanaomzunguka karibu yake.
Yanga ni wawakilishi ni pekee hapa ukanda wa Afrika Mashariki na Tanzania kwa wakati huu kuwa ni kilabu pekee ambayo inatuwakilisha katika michuano ya kombe la shirikisho katika bara la Afrika na tunajivunia kwani ni fursa pekee ya kutangaza Taifa letu kimataifa pia inatoa hamasa kwa timu zingine kujituma zaidi ili tu waweze kufikia malengo stahiki katika Tasnia ya maendeleo ya mpira wa miguu.
Yanga imefanikiwa kuingia katika raundi ya pili katika michuano hiyo ya shirikisho barani Afrika na hii imechagizwa na mara baada ya kuwatoa Fc. Platinum kutoka nchini Zimbabwe kwa jumla ya magoli 5-2 ikiwa ni ushindi mmoja mnono sana hasa katika michuano mizito kama hii.
Kumbuka Yanga iliitoa pia BDF XI katika hatua ya awali kutoka Botswana na hiyo ni hatua mojawapo ambayo timu iliisaidia kusimama na kutoa motisha kubwa na kuijenga katika hali ya matokeo zaidi ndiyo maana hadi sasa tunaiona Yanga ikiwa katika hatua nyingine tofauti kuingia raundi ya pili.
Licha ya hayo yote na pongezi nilizozitoa Yanga sasa inabidi iwe na fikra zingine upande wa pili juu ya utamaduni wa waarabu jinsi walivyo pindi timu zetu haswa kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki tunapopangiwa nao, wamekuwa ni watu wa fitina, watu wasio na huruma kabisa haswa unapoenda nchini kwao kwaajili ya mechi.
Kuna uwezekano mzuri wa Yanga kufanya vyema katika mechi ya awali ambayo wamebahatika kupangiwa nyumbani kati ya tarehe 14 au 15 mwezi huu ambapo watakutana na Etou du Sahel waarabu hawa kutoka Tunisia, timu ambayo alicheza Mganda Emmanuel Okwi akitokea katika kilabu ya Simba.
Kufanya vyema kwa Yanga katika dimba la hapa kwetu sio tija ya wao kufanya vizuri pindi watakapoenda kule kwao, waarabu wamekuwa ni watu wa fitina na huwa wanafanya mikakati na mbinu mbalimbali ili kuweza kuwaondoa kabisa katika hamasa nzuri ya mchezo na wanakufunga hukohuko wakiwa nyumbani kwao.
CAF haijaweka msimamo wa kwamba ni lazima timu inapokwenda ugenini iandaliwe mahitaji yote na timu mwenyeji jambo ambalo linaweza kutoa nafasi kwa timu ngeni kujiwekea maandalizi yake binafsi bila kuwategema wenyeji kwa kila kitu pindi watakapoenda kule kwao na hili litakuwa ni faida kwa Yanga.
Ninachowaomba viongozi wa Yanga pamoja na benchi la ufundi wa ujumla wasiwe na shaka juu ya hilo kwani mazoezi nii njia nzuri ya maandalizi kuweza kufikia lengo husika, wake wajitume mazoezini na wasifikirie sana ni kipi wataenda kufanyiwa na waarabu na asilimia kubwa ya sisi Watanzania wapenda soka tunapoenda kule tunakuwa ni watu wa kulalamika kuhusu fitina tu.
Umuhimu wa viongozi katika benchi lao la ufundi ni kuhakikisha timu inapata kila mahitaji kwa ujumla wa wachezaji na sio mchezaji mmoja mmoja ili kutoshusha ari na amsha-amsha ya timu uwanjani na kujenga umoja na kila mmoja kucheza akiwa na morali pia motisha ya kupata matokeo tu uwanjani.
Ni vizuri pia kama uongozi ukituma baadhi ya watu kule kimyakimya waende kufuatilia baadhi ya mechi wanazocheza, mbinu za mazoezi wanazozitumia halikadhalika kuweza kupeleleza ni kipi haswa wanakifanya pindi wanapokuwa nje ya uwanja ili kuweza kupata moja moja kwa jawabu na hii itafungua njia nzuri kwa Yanga kutupa raha Watanzania siku ya mwisho, sio vibaya pia kama wakipata video za michezo yao ya nyuma nalo litasaidia pia.
Yanga kama kilabu inapaswa kutambua kuwa wale jamaa zetu Waarabu wana mtindo wa kufanya mbinu na kutuma wapelelezi kuja kufanya uchunguzi wa kile kinachofanyika huku na hili sio kwa waarabu tu bali hata kule barani Ulaya makocha na viongozi wa benchi la ufundi wamekuwa wakifanya haya.
Mwisho namaliza kwa kusema wachezaji wanatakiwa kutambua kuwa sisi wapenzi na mashabiki tuna uchu wa kuona timu zetu zikiendelea na hatuna haja ya kuweka tofauti pindi tunapoenda kucheza kimataifa, habari za Usimba na Uyanga tunazitupilia pembeni na sasa ni wao wanatakiwa kujua ni machungu yapi ambayo huwa tunayapata pindi timu zetu zinapoishia pale ambapo hapastahili.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!