Searching...
Image and video hosting by TinyPic
20 December 2014
Saturday, December 20, 2014

Uchambuzi: Stoke City vs Chelsea


Na Chikoti Cico

Mchezo mmoja wa ligi kuu nchini Uingereza utachezwa siku ya Jumatatu ambapo timu ya Stoke City itaikaribisha timu ya Chelsea kwenye uwanja wao wa Britannia huku kila timu ikitafuta alama tatu muhimu.

Stoke City mpaka sasa wanashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 19 hivyo watahitaji matokeo mazuri kwenye mchezo huo na kama wakishinda wanaweza kupanda mpaka nafasi ya tisa.

Kocha wa Stoke City Mark Hughes anatarajia wachezaji wake Bojan Krkic na Marc Muniesa ambao walikuwa majeruhi kuweza kucheza mchezo huo huku pia akitarajia Stephen Ireland ambaye aliumia goti kuweza kuwa fiti kucheza dhidi ya Chelsea.

Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha Stoke wamekuwa na rekodi mbaya dhidi ya Chelsea kwani katika michezo 12 iliyopita Stoke imeshinda mchezo mmoja tu na kufungwa michezo tisa huku ikitoka sare michezo miwili.

Pia takwimu zinaonyesha Stoke wamekuwa na rekodi nzuri ya kutofungwa michezo sita iliyopita ya ligi iliyochezwa siku ya Jumatatu huku wakishinda michezo miwili na kutoka sare michezo minne.

Kikosi cha Stoke City kinaweza kuwa hivi: Begovic, Bardsley, Shawcross, Wilson, Pieters, Nzonzi, Cameron, Diouf, Bojan, Walters, Crouch

Kwa upande wa Chelsea ambao wanaongoza ligi wakiwa na alama 39 wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo kutafuta alama tatu muhimu ili kuendelea kujikita kileleni mwa ligi kuu nchini Uingereza, mpaka sasa wamepishana kwa alama tatu tu na Manchester City wanaoishika nafasi ya pili wakiwa na alama 36.

Kocha wa Chelsea Jose Mourinho kuelekea mchezo hana wachezaji ambao ni majeruhi huku kipa Thibaus Courtois akitarajiwa kurejea golini baada ya kukosa michezo miwili iliyopita, Didier Drogba na Kurt Zouma ambao waliumia kwenye mchezo wa Capital One dhidi ya Derby nao wanaendelea vyema.

Kuelekea mchezo huo timu ya Chelsea inaonekana kuwa na takwimu nzuri kwa mechi zilizochezwa siku ya Jumatatu kwani katika michezo 19 iliyopita ya ligi iliyochezwa siku ya Jumatatu imeshinda michezo 11 na kutoka sare michezo saba huku ikifungwa mchezo mmoja.

Pia takwimu zinaonyesha kiungo wa Chelsea Eden Hazard hajawahi kufunga goli hata moja kwenye mechi yoyote ya ugenini toka Januari 11 mwaka huu huku magoli yake yote 11 yaliyopita katika mashindano mbalimbali akiyafunga kwenye uwanja wa Stamford Bridge.

Kikosi cha Chelsea kinaweza kuwa hivi: Courtois; Ivanovic, Cahill, Terry, Azpilicueta; Fabregas, Matic; Willian, Oscar, Hazard; Costa.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!