KOCHA AKUBALI KUBWAGA MANYANGA EPL
Gus Poyet ametishia kung'atuka mamlakani kama meneja wa klabu ya ligi ya Premier ya Uingereza, Sunderland, ikiwa atahisi kuwa wachezaji wake wamesalimu nia ya kupigania hadhi yao kwenye shindano hilo.
Sunderland waligongwa 2-1 na West Ham Jumatatu usiku kufikisha mechi yao ya 17 kucharazwa msimu huu huku wakisalia nafasi ya 19 na moja tu kutoka mkia na alama 25 pekee, pointi nne nyuma ya West Bromwich Albion wanaomiliki nafasi ya 17 na ya mwisho kuhakikisha usalama kwenye ligi hiyo.
Ingawa wamecheza mechi mbili chache ikilinganishwa na Fulham wanaovuta mkia na Cardiff walio mbele yao katika nafasi ya 18, Sunderland watakuwa na wiki tatu ngumu pale watakapo menyana na Tottenham Hotspur, Everton, Manchester City na Chelsea wanaopaa nafasi za sita bora katika Premier.
Maasimu wao wa kung'ang'ania uhai katika daraja kuu, West Brom na Crystal Palace, wamecheza mechi moja zaidi ya timu inayojulikana kwa utani kama, Black Cats.
Huku wakikosa kutamba tangu wawaadhibu watani wao wa jadi, Newcastle, 3-0 mwanzo wa Februari, hatima ya Sunderland yaweza kutambulika hata kabla ya msimu kukamilika.
“Ikiwa timu yangu itainua mikono, nitaondoka,” meneja wao, raia wa Uruguay, Gus Poyet, ambaye aliwika enzi zake kama mchezaji aliwaambia wanahabari.
“Hakuna haja ya yeyote kunifuta, nitaondoka mwenyewe, sawa?” aliendelea. “Ukiona timu hii ikifa moyo kabla ya mwisho wa msimu, hutaniona hapa.”
Poyet alirithi Mtaliano Paulo Di Canio huku Sunderland wakiwa wa mwisho katika kwenye msimamo wa ligi kabla ya kuongeza juhudi zilizoleta uhai pale walipowania fainali ya kombe la Capital One ambapo walibwagwa na City na robo fainali za lile la FA.
0 comments:
Post a Comment