Searching...
Image and video hosting by TinyPic
21 February 2015
Saturday, February 21, 2015

Bayern Munich yaendeleza ubabe Bundesliga






Na Florence George


Baada ya kutoka suluhu na timu ya Shakhtar Donetsk katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 wa klabu bingwa ulaya(UEFA) klabu ya soka ya Bayern Munich imeendelea kugawa vipigo kwa timu za ligi kuu nchini Ujerumani baada ya kuinyuka magoli 6-0 timu ya SC Paderborn 07 hiyo jana.

Katika mchezo huo mshambuliaji wa kimataifa wa Poland Robert Lewandowski ndio alikuwa wa kwanza kuifungia timu yake dakika ya 24 kabla ya kuongeza la pili dakika nane kabla ya mapumziko kufuatia krosi nzuri kutoka kwa Frank Ribery.

Paderborn walilazimika kucheza dakika 27 za mwisho wakiwa 10 uwanjani baada ya Florian Hartherz kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Arjen Robben katika eneo la hatari na mwamuzi kuwazawadia Bayern penati ambayo ilifungwa na Robben na kufanya matokeo yasomeke 0-3.

Bayern waliendelea kulishambulia goli ya wenyeji wao na kufanikiwa kufunga magoli mengine matatu yaliyofungwa na Ribery,Mitchell Weiser na Robben akikamilisha kapu hilo la magoli.

Kipigo hicho kilikuwa cha pili kwa ukubwa Bayern kutoa tangu mwaka huu uanze kwani wiki iliyopiga vijana hao wa Pep Guardiola waliivurumisha timu ya Hamburg magoli 8-0.

Bayern Munich imeendelea kujichimbia kileleni mwa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 55 katika michezo 22 iliyocheza,pointi 11 mbele ya klabu ya  Wolfsburg iliyonafasi ya pili ambayo inatarajiwa kucheza leo hii dhidi ya Hertha Berlin .

 

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!