Yanga yaisambaratisha Jang'ombe huko Zanzibar
Na Oscar Oscar Jr
Mabao matatu (Hat-Trick) yaliyofungwa na Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva na bao la jioni kutoka kwa Kpah Sherman yalitosha kuwapatia ushindi mnono watoto wa Jangwani timu ya Yanga kwenye mchezo wao wa kwanza kwenye kombe la Mapinduzi walipovaana na timu ya Taifa ya Jang'ombe.
Mchezo huo ulishuhudia Yanga wakitawala kwa kiasi kkubwa kwenye kila idara na hasa katika kumilika mpira kutokana na kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm kuwaanzisha wachezaji wenye kasi.
Hans alianza na Mrisho Ngassa, Andrey Coutinho, Simon Msuva, Hassan Dilunga na Salum Telela kwenye kiungo kitu kilichowawia vigumu vijana wa Jang'ombe kutawala mchezo huo.
Pamoja na mabao hayo ya Yanga, bado safu ya ulinzi hasa mabeki wa kati walionekana kufanya makosa mara kadhaa ambapo Nahodha Nadir Haroub alicheza na Pato Ngonyani na kama washambuliaji wa Jang'ombe wangekuwa makini, wangeweza kujipatia mabao hasa kipindi cha kwanza.
Matokeo hayo yanakamilisha idadi ya timu nne zinazoshiriki michuano hiyo kutoka Tanzania bara kukamilisha mzunguko wa kwanza wa makundi hayo huku Simba ikiwa ndiyo timu pekee ambayo haina alama hata moja baada ya hapo jana kufungwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar huku Azam Fc kwenye mchezo wa mapema leo wakitoka sare ya bao 2-2 na KCCA ya Uganda.
0 comments:
Post a Comment