Searching...
Image and video hosting by TinyPic
1 January 2015
Thursday, January 01, 2015

Uchambuzi: Southampton vs Arsenal


Na Chikoti Cico

Nyasi za uwanja wa ST Mary’s zitawaka moto kwa mchezo wa ligi kuu nchini Uingereza kati ya Southampton dhidi ya Arsenal, mchezo unaotarajiwa kuwa wa kusisimua na wenye ushindani huku kila timu ikitafuta alama tatu muhimu.

Baada ya kutoka sare ya goli 1-1 na vinara wa ligi ya Uingereza timu ya Chelsea, Southampton wataingia kwenye mchezo huku wakishika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi huku wakiwa na alama 33 sawasawa na Arsenal.

Kocha wa Southampton Mdachi Ronald Koeman kuelekea mchezo huo atamkosa kiungo wake mahiri Morgan Schneiderlin ambaye alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Chelsea.

Ryan Bertrand ambaye hakucheza mchezo uliopita kwasababu Chelsea ni timu yake mama na yuko kwa mkopo Southampton, anatarajiwa kurejea kikosini kwenye mchezo huo dhidi ya Arsenal maarufu kama “washika bunduki wa jiji la London”.

Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha Southampton hawajashinda katika michezo 10 iliyopita ya ligi dhidi ya Arsenal huku wakifungwa michezo sita na kutoka sare michezo minne.

Wakati huo huo, takwimu zinaonyesha kumekuwa na kadi tano nyekundu katika michezo sita iliyochezwa kwenye uwanja wa St Mary’s kati ya Southampton dhidi ya Arsenal

Kikosi cha Southampton kinaweza kuwa hivi: Forster; Yoshida, Fonte, Alderweireld, Bertrand; Ward-Prowse, Wanyama, Davis; Tadic, Pelle, Mane

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger kwenye mchezo huo atawakosa Aaron Ramsey, Mikel Arteta, Mesut Ozil, Abou Diaby, Jack Wilshere na Serge Gnabry ambao ni majeruhi huku Olivier Giroud akiendelea kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu.

Wakati huo huo Danny Welbeck ana hatihati ya kutokucheza mchezo huo baada ya kuumia hivyo safu ya ushambuliaji ya Arsenal inaweza kuongozwa na Theo Walcott ama Lukas Podolski.

Baada ya kuifunga timu West Ham kwa magoli 2-1 kwenye mchezo uliopita na kufikisha alama 33 huku wakishika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi Arsenal wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo kutafuta alama tatu muhimu zitakazowarejesha “top four”.

Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha katika michezo 10 ya siku ya mwaka mpya, Arsenal iliyocheza kwenye historia ya ligi kuu nchini Uingereza imeshinda michezo saba na kufungwa mchezo mmoja huku ikitoka sare michezo miwili.

Kikosi cha Arsenal kinaweza kuwa hivi: Szczesny; Debuchy, Koscielny, Mertesacker, Gibbs; Cazorla, Flamini, Coquelin; Oxlade-Chamberlain, Sanchez, Rosicky

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!