Uchambuzi: Ndanda Fc vs Polis Moro: Nangwanda Sijaona Stadium.
Na Oscar Oscar Jr
Ligi kuu Tanzania bara inatarajia kuendelea tena wikendi hii kwa michezo mitatu ambapo siku ya Jumamosi kutakuwa na michezo miwili kwenye viwanja tofauti na Jumapili, utapigwa pia mchezo mwingine.
Ndanda Fc ambao wameshinda michezo mitatu ila kati ya hiyo ni mchezo mmoja tu walishinda wakiwa katika uwanja wa nyumbani, Jumamosi hii watawakaribisha maafande wa Polis kutoka mkoa wa Morogoro kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona, mkoani Mtwara.
Mchezo uliopita Ndanda wakiwa ugenini kwenye dimba la Sokoine walifanikiwa kuonda na alama tatu baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons na kupanda hadi kwenye nafasi ya 11 ya msimamo wa ligi kuu.
Polis Morogoro ambao wanakamata nafasi ya tano wakiwa na alama 13, waliweza kujipatia alama nne kwenye mechi mbili za hivi karibuni kuwalaza mabao 2-0 Mgambo JKT na kutoka sare pacha na Stand United kutoka mkoa wa Shinyanga.
Hizi ni timu ambazo zimepanda daraja msimu huu na kwa hali hiyo hakuna timu itakayokuwa inamuogopa mwenzie kitendo ambacho kitapelekea kuchezwa kwa mpira wa wazi.
Hapo awali mchezo uliowakutanisha Stand United dhidi ya Ndanda F timu zilizopanda daraja, tulishuhudia magoli matano yakifunga huku Ndanda wakiibuka na ushindi wa bao 4-.1.
Mchezo mwingine wa aina hiyo baina ya Polis Moro dhidi ya Stand United, haukuwa na goli hata moja licha ya timu hizo kugawana vipindi vya kutawala mchezo.
Ushindi waliopata Ndanda Ugenini inaweza kuwa chachu kwao ya kutafuta ushindi wao wa nne msimu huu pale watakapoumana na Polis Morogoro.
Kwa uande wa takwimu, Ndanda ndiyo timu yenye safu butu ya ulinzi kwani mpaka sasa wao ndiyo wameruhusu kufungwa magoli mengi zaidi kuliko timu yoyote (14) huku wakifunga mabao tisa. Polis Morogoro ambao wanakamata nafasi ya tano, wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara saba huku wao wakifunga mabao nane.
0 comments:
Post a Comment