Na Chikoti Cico
Unaweza kusema ni vita ya Wadachi kati ya Louis van Gaal dhidi ya Ronald Koeman katika mchezo utakaopigwa kwenye uwanja wa Old Trafford kati ya Manchester United dhidi ya Southampton, mchezo unaotarajiwa kuwa wa kusisimua kwani timu hizi mbili zimepishana kwa alama moja tu kwenye msimamo wa ligi.
Manchester United wanaoshikilia nafasi ya tatu wakiwa na alama 37 kwenye msimamo wa ligi wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo kutafuta alama tatu muhimu na kuzidi kuzikimbiza Manchester City na Chelsea kileleni.
Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal kwenye mchezo huo atamkosa Ashley Young ambaye aliumia kwenye mchezo wa mwaka mpya dhidi ya Stoke City na hivyo anatarajiwa kuwa nje kwa muda wa wiki nne mpaka sita huku kipa mpya wa timu hiyo Victor Valdes akitarajiwa kuwepo kikosini.
Wachezaji wengine wa United; Rafael, Luke Shaw, Marcos Rojo, Daley Blind, Maroune Fellaini na Antonio Valencia ambao walikuwa majeruhi kwasasa wanaendelea vizuri kuelekea mchezo huo dhidi ya Southampton.
Kwenye mchezo huo takwimu zinaonyesha United hawajafungwa katika michezo 10 iliyopita ya ligi huku wakishinda michezo saba na kutoka sare michezo mitatu.
Pia takwimu zinaonyesha mshambuliaji wa United Robin van Persie amefunga magoli saba katika mechi saba alizocheza dhidi ya Southampton kwenye ligi.
Kikosi cha kocha Van Gaal kinaweza kuwa hivi: De Gea; Jones, Smalling, Evans; Shaw, Carrick, Rooney, Di Maria; Mata; Van Persie, Falcao.
Kwa upande wa Ronald Koeman kocha wa Southampton, kwenye mchezo huo atawakosa Sadio Mane, Jay Rodriguez na Sam Gallagher ambao ni majeruhi pia mlinzi Maya Yoshida atakosekana baada ya kwenda kushiriki michuano ya kombe la Asia na timu ya taifa ya Japan.
Pia kocha huyo ataweza kuwajumuisha kikosini Nathaniel Clyne na Jack Cork ambao walikuwa majeruhi huku Eljero Elia aliyesajiliwa kwa mkopo kutoka Werder Bremen pia akitarajiwa kuwepo kikosini kwa mara ya kwanza toka aliposajiliwa.
Mpaka sasa Southampton wanashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 36.
Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha Southampton wamefungwa michezo sita na kutoka sare michezo miwili kati ya michezo minane iliyopita waliyocheza dhidi ya Man United.
Pia takwimu zinaonyesha kiungo wa Southampton James Ward-Prowse ametoa pasi tatu za magoli yaani “goal assist” katika michezo mitatu iliyopita ya ligi.
Kikosi cha kocha Koeman kinaweza kuwa hivi: Forster; Alderweireld, Fonte, Clyne, Bertrand; Wanyama, Davis, Ward-Prowse; Tadic, Elia; Pelle
0 comments:
Post a Comment