Searching...
Image and video hosting by TinyPic
9 January 2015
Friday, January 09, 2015

Uchambuzi: Arsenal vs Stoke City Jumapili saa 10:30 Jioni.


Na Chikoti Cico

Mchezo wa raundi ya kwanza kwenye uwanja wa Britannia kati ya timu hizi mbili uliisha kwa Stoke City kushinda kwa magoli 3-2 hivyo mchezo huo unatarajiwa kuwa wa piga nikupige timu hizi zitakaporejeana siku ya Jumapili kwenye uwanja wa Emirates ambapo Arsenal watataka kulipiza kisasi.

Kwenye mchezo huo kocha wa Arsenal Arsene Wenger atawakaribisha Aaron Ramsey na Mesut Ozil ambao walikuwa majeruhi pia Olivier Giroud ambaye alikuwa akitumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu.

Wakati huo huo kocha huyo ataamua kati ya makipa Wojciech Szczesny na David Ospina nani atakuwa langoni kwenye mchezo huo lakini atawakosa Danny Welbeck, Mikel Arteta, Abou Diaby na Jack Wilshere ambao bado ni majeruhi.

Mpaka sasa timu ya Arsenal inashika nafasi ya sita ikiwa na alama 33 kwenye msimamo wa ligi huku wakifuga mabao 34 na kuruhusu 25.

Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha timu ya Arsenal imeshinda michezo 18 na kufungwa michezo nane huku wakitoka sare mchezo mmoja katika michezo 27 ya ligi kwenye uwanja wa Emirates.

Pia, takwimu zinaonyesha Arsenal imeruhusu nyavu zao kutikiswa katika michezo sita iliyopita ya ligi yani hawana “clean sheet”  hata moja katika michezo hiyo.

Kikosi cha Arsenal kinaweza kuwa hivi: Szczesny; Debuchy, Mertesacker, Koscielny, Gibbs; Flamini, Ramsey; Oxlade-Chamberlain, Cazorla, Sanchez; Giroud.

Kwa upande wa Stoke City ambao wanashika nafasi ya 11 wakiwa na alama 26 kwenye msimamo wa ligi wataingia kwenye mchezo huo zaidi wakitarajiwa kutumia mipira mirefu kutafuta ushindi dhidi ya Arsenal kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza.

Kocha wa Stoke City, Mark Hughes ana wachezaji wa tatu ambao walikuwa majeruhi na wanatarajiwa kurejea kikosini ambao ni Marc Muniesa, Victor Moses na Bojan Krkic pia mlinzi Philipp Wollscheid aliyesajiliwa kwa mkopo akitokea Bayern Leverkusen anaweza kucheza mchezo huo.

Lakini atamkosa mshambuliaji wake Mame Biram Diouf aliyeenda kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika huku pia mchezaji mwingine Marc Wilson akiwa na hatihati ya kutokucheza mchezo huo.

Stoke City kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha wamefungwa na Arsenal michezo 12 mfululizo iliyochezwa nyumbani kwa Arsenal, pia takwimu zinaonyesha mshambuliaji wa Stoke Peter Crouch ameifunga Arsenal magoli manane ikiwa ni moja ya timu alizozifunga magoli mengi.

Kikosi cha Stoke City kinaweza kuwa hivi: Begovic; Cameron, Shawcross, Muniesa, Pieters; N'Zonzi, Whelan; Arnautovic, Walters, Krkic; Crouch

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!