Timu ya wananchi haikamatiki kwa sasa.
Na Oscar Oscar Jr
Watoto wa Jangwani wanaonekana hawakamatiki kwenye michuano ya Mapinduzi inayoendelea huko visiwani Zanzibar baada ya leo kibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Polis ya Zanzibar.
Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil, Andrey Coutinho akitupia bao mbili huku Kpah shermann kutoka nchini Liberia na Simoni Msuva wakipiga bao moja kila mtu na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo kulipukwa na shangwe
Pengine hiki ndicho walichokuwa wanakihitaji wana Jangwani baada ya kufanya usajili mzuri na kubadilisha benchi la ufundi kwa kumrejesha "Babu" kocha Hans Van Der Pluijm ambaye msimu uliopita aliwakosha wana wa Yanga pale alipokuwa anatoa dozi ya bao kuanzia nne kwa wapinzani kwenye michezo kadhaa.
Yanga sasa wametimiza alama sita kwenye kundi lao baada ya mchezo uliopita kuibuka pia na ushindi kama huo huku wakiwa hawajaruhusu hata bao moja kutinga kwenye nyavu zao.
Michezo ya awali leo ilishuhudia mabingwa watetezi timu ya KCCA kutoka nchini Uganda wakipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mtende ya Zanzibar huku Taifa ya Jang'ombe wakiibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya timu ya Shaba.
Kwa matokeo hayo, Yanga tayari wameshatinga kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo na wanachosubiri ni kukamilisha tu mechi yao ya mwisho kwenye hatua za makundi ambapo watakamilisha na timu ya Shaba.
0 comments:
Post a Comment