Na Samuel Samuel - 0652464525
Timu ya Shaba ikiwa na viungo wepesi na washambuliaji wasio na kasi sana kama ilivyo kwa wakongwe wa Yanga iliwabana mbavu Polisi hao wenye uchu na kuambulia ushindi kiduchu wa goli moja bila.
Polisi Zanzibar inayosifika kwa soka safi la kutumia viungo wengi leo watakwaana uso kwa uso na jeshi kakamavu la Hans Pluijm kocha mkuu wa klabu hiyo toka jijini Dar.
Wakati Polisi wakiingia uwanjani na kumbukumbu ya ushindi wa goli moja bila, Yanga inaivaa timu hiyo kifua mbele ikiwa na pointi tatu kibindoni baada ya kuishushia gharika ya magoli timu ya Taifa Jang'ombe .
Yanga ilishinda 4-0 huku kiungo wake machachari Saimoni Msuva akifunga magoli matatu peke yake. Ingawa Yanga ilishinda mchezo uliopita hiyo sio tiketi ya kujihakikishia ushindi mnono mbele ya Polisi.
Tahadhari kubwa inahitaji hasa ukiitazama safu ya ulinzi ya Polisi iliyoimarika vizuri kwa kuwa na mabeki warefu, wenye kuelewana na maamuzi ya haraka kuondosha hatari langoni kwao. Pluijm kama ataendelea kumuamini Salumu Telela pale kati na kumuanzisha Haruna Niyonzima kule mbele basi Yanga itaimarika zaidi kuliko mechi iliyopita.
Bado Dilunga hajaimarika kama kiungo mchezeshaji kwenye mechi zenye ushindani mkubwa kama ya Leo. Polisi ni lazima wamchunge sana Msuva kiungo anayezidi kutakata kila uchao, Msuva ni fundi wa maamuzi ya haraka na kuichachafya beki ya wapinzani muda wote.
Tunatarajia kiungo mshambuliaji Andrey Coutinho ataendelea kupewa nafasi leo kutokana na soka safi alilolionesha mechi iliyopita. Ameonesha kujiamini na kucheza kitimu zaidi .
Mchezo huu utakuwa mzuri na wa kusisimua sana kutokana na hamasa pande zote mbili. Wadau wengi wa soka wanaipa nafasi Yanga kutokana na safu yake ya ushambuliaji ilivyo moto wa kuotea mbali. Yanga ina magoli manne kwenye mechi moja wakati Polisi ina goli moja tu . zote hazijafungwa.
0 comments:
Post a Comment