Prisons hoi kwa Ndanda Fc huko Mbeya.
Na Oscar Oscar Jr
Mgambo JKT na timu ya Ndanda Fc pengine ndiyo timu za kuchungwa zaidi kwani zinashikilia rekodi ya kutotoka sare hata mchezo mmoja kwenye ligi kuu Tanzania bara ambayo imefika kwenye mzunguko wa tisa kwa timu ambazo hazishiriki michuano ya Mapinduzi Cup inayoendelea huko Visiwani Zanzibar.
Maana yake ni kwamba, unapokutana na moja kati ya timu hizo, ukishindwa kuwafunga, wao watakusambaratisha.
Ndanda leo hii wameweza kujipatia ushindi wao wa tatu kwenye mchezo waliocheza ugenini kwenye dimba la Sokoine kwa kuwachapa Mafande wa Magereza, Tanzania Prisons kwa bao 1-0 na kujiongezea alama tatu muhimu na sasa wanatimiza alama tisa na kujinasua mkiani kwenye msimamo wa ligi kuu.
Tanzania Prisons ambao msimu uliopita walilazimika kusubiri matokeo ya mechi yao mwisho ili kusalia kwenye ligi kuu na kwa hali ilivyo kwa sasa, kunauwezekano wakaelekea kule walikotoka msimu uliopita kwasababu kwa sasa wao ndiyo wanakamata mkia.
Matokeo haya kwa Ndanda yanamuweza kocha Abdul Mingange kwenye hali nzuri kwani katika mechi tano alizowaongoza Ndanda, wamepoteza michezo mitatu na kuibuka na ushindi mara mbili.
Kwa sasa Ndanda wanarejea Mtwara kwenda kuwasubiri Polis Morogoro kwenye mchezo wa mzunguko wa 10 utakaopigwa wiki ijao kwenye dimba la Nangwanda Sijaona.
Baada ya kushindwa kuutumia vema uwanja wa nyumbani kwenye michezo miwili mfululizo, Tanzania Prisons, watakuwa na safari ya kuelekea Morogoro kwenda kupambana na vinara wa ligi kuu Mtibwa Sugar ambao kwa sasa wako Zanzibar kwenye michuano ya Mapinduzi Cup.
0 comments:
Post a Comment