Said Bahanuzi afungua akaunti ya magoli huko Mtwara.
Na Oscar Oscar Jr
Mchezo wa ligi kuu Tanzania bara kati ya Ndanda Fc dhidi ya Polis Morogoro umemalizika kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 1-1 huku mshambuliaji wa Yanga ambaye anakipiga na Polis Moro kwa mkopo, Said Bahanuzi akifungua akaunti ya magoli kwa kufunga bao moja kwenye mchezo huo.
Kwa mara ya kwanza Ndanda Fc wamelazimishwa sare kwenye ligi kuu kwani kabla ya mchezo wa leo, walikuwa wameshinda mechi tatu na kupoteza mechi sita pasipokuwa na sare hata moja.
Kocha Abdul Mingange anaonekana kuwa na mwenendo mzuri tangu alipoichukuwa Ndanda Fc ambayo ilimtimua kocha wake wa awali, Dennies Kitambi baada ya mechi nne tu za awali.
Kwa matokeo hayo, Polis Moro wamefikisha alama 14 ambazo ni sawa na Kagera Sugar, Yanga na Azam ingawa Polis amecheza mechi nyingi zaidi ya hizo timu nyingine.
Akizungumza na SOKA STADIUM, Meneja wa timu ya Polis Moro, Afredy Lwambano amesema kuwa timu itarejea Morogoro hapo kesho kujiandaa na mchezo wao unaofuata dhidi ya Coasta Union utakaopigwa mkoa wa Tanga.
"Tunashukuru tumepata sare huku Said Bahanuzi akifunga bao hilo na kesho tunajiandaa kuweza kurejea Morogoro kwa ajili ya kujipanga kwa mchezo wetu unaofuata dhidi ya Coastal Union mkoani Tanga"
Akizungumzia kiwango cha Bahanuzi Lwambano amesema " Bahanuzi alikuwa kwenye kiwango bora kabisa na kama angetulia angeweza kufunga hata mabao matatu lakini tunashukuru kwa alama moja tulioipata"
Kwa upande wa Ndanda, matokeo haya yamewafanya kucheza mechi mbili mfululizo kwa mara ya kwanza bila kupoteza baada ya wiki iliyopita kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons na sasa wametimiza alama 10.
0 comments:
Post a Comment