Na Oscar Oscar Jr
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi huenda amegeuka kuwa "mtoto wa Kariakoo" baada ya utata kuibuliwa na gazeti la Mwanaspoti kuhusiana na mizengwe yake.
Kulikuwa na taarifa kuwa mchezaji huyo ameruhusiwa kwenda kwao kuendelea na fungate kutokana na mchezaji huyo hivi karibuni kufunga ndoa ya kimila nyumbani kwao.
Gazeti la mwanaspoti la leo, limeandika kuwa mchezaji huyo wala hakwenda kwao na badala yake ameendelea kubakia ndani ya Dar es salaam wakati timu yake ikitaabika huko Zanzibar inakoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi na tayari jana wamefungwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar.
Taarifa kutoka kwenye gazeti hilo inasema " Rafiki wa karibu na Okwi, alilithibitishia Mwanaspoti kuwa, mchezaji huyo hakwenda Uganda japokuwa aliomba ruhusa hiyo na viongozi kumruhusu lakini aliamua kufanya hivyo kwa sababu zake binafsi"
Bado haijafahamika sababu zilizopelekea mchezaji huyo kutokwenda kwao wala kuungana na timu iliyoko visiwani Zanzibar ingawa baadhi ya wachezaji wenzie ambao ni raia wa Uganda, wao wameamua kurudi kwako kutokana na malipo yao ya usajili kutokamilika.
Simba hadi mzunguko wa nane wa ligi kuu unamalizika, imejikuta ikikaa kwenye nafasi ya 10 huku wakiwa na alama tisa pekee baada ya kutoka sare mara sita, kushinda mchezo mmoja na kupoteza mmoja.
Aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Patrick Phiri ameendelea kubaki njia panda kutokana na kuenea taarifa za kusitishwa kwa kibarua chake huku kocha anayetajwa kuchukuwa nafasi yake ameshatua nchini na mazungumzo na uongozi wa Simba yanaendelea.
0 comments:
Post a Comment