Searching...
Image and video hosting by TinyPic
29 January 2015
Thursday, January 29, 2015

Guinea yatinga robo fainali kiaina.


Na Chikoti Cico

Timu ya taifa ya Guinea imeingia hatua ya robo ya michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika baada ya jina lao kuchaguliwa wakati wa droo ya bahati nasibu iliyofanyika jijini Malabo nchini Guinea ya Ikweta katika kutafuta mshindi wa pili kwenye kundi D baada ya timu hizo mbili kutoka sare kwenye mchezo wao wa mwisho na hivyo wote kuwa na alama sawa na tofauti sawa ya magoli ya kufunga na kufungwa.
Kutokana na matokeo ya droo hiyo Guinea itacheza na Ghana kwenye hatua ya robo fainali huku Mali ikirejea nyumbani ikiwafuata Kameruni ambao wameshayaaga mashindano hayo baada ya kufungwa na Ivory Coast kwa goli 1-0 na kushika mkia kwenye msimamo wa kundi D.
Mkurugenzi wa Fedha kutoka Wizara ya michezo ya Guinea Amara Dabo ambaye alishiriki kwenye droo hiyo akiongea baada ya droo hiyo alisema “Bahati ya miungu wa soka imetabasamu kwetu, ilikuwa ni safari ndefu mpaka sasa”
Katika droo hiyo wawakilishi wa kila nchi walitoa mpira kutoka kwenye bakuli na Raisi wa chama cha soka cha nchini Mali Boubacar Diarra alikuwa wa kwanza kufanya hivyo na ambaye alitoa mpira ambao uliwaweka Mali kwenye nafasi ya tatu na kutoka kwenye michuano hiyo na ndipo Dabo alipotoa mpira ambao uliihakikishia Guinea nafasi ya pili nyuma ya Ivory Coast kwenye msimamo wa kundi D.
“Bahati mbaya inabidi tuzigawanye timu mbili ambao ziko sawa, zilizoungana kiusahihi lakini ilibidi hakuna njia nyingine bali kuendelea na droo ya bahati nasibu” alisema raisi wa shirikisho la soka la Afrika (CAF) Issa Hayatou kwenye droo hiyo nchini Guinea ya Ikweta.
Hii ni mara ya tatu kwenye historia ya kombe la Mataifa ya Afrika kwa timu mbili kutenganishwa kupitia droo ya bahati nasibu baada ya hatua ya makundi. Mwaka 1972 na 1988 bahati ya droo hiyo iliwaangukia Congo na Algeria.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!