Searching...
Image and video hosting by TinyPic
14 January 2015
Wednesday, January 14, 2015

Makala: Ballon d’Or na kura za kinafki, kirafiki na kiutaifa.




Na Chikoti Cico

Javier Mascherano ni mchezaji bora duniani kuliko Christiano Ronaldo na Lionel Messi na Manuel Neuer, Thibaut Courtois ni mchezaji bora duniani kuliko Ronaldo, Messi na Neuer na Gareth Bale pia ni mchezaji bora duniani kuliko Ronaldo, Messi na Neuer.

Najua utashangaa nini hiki mbona mshindi wa tuzo ya mchezaji bora duniani yaani Ballon d’Or kwa mwaka 2014 tayari inajulikana ni Christiano Ronaldo. 

Ndiyo kwa sehemu kubwa ya wapiga kura wa tuzo hiyo Ronaldo ni mchezaji bora wa duniani tena kwa asilimia 37.66 akifuatiwa na Messi kwa asilimia 15.76 na Manuel Neuer asilimia 15.72.

Lakini machoni kwa kocha wa timu ya taifa ya Uingereza Roy Hudgson, Javier Mascherano ndiyo mchezaji bora duniani zaidi ya Ronaldo na hata Messi.

Nahodha wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Vicent Kompany nae pia machoni kwake Courtois ndiye mchezaji bora duniani na kwa kocha wa timu ya taifa ya Wales Chris Coleman, Bale ndiye mchezaji bora duniani.

Hivyo ndivyo chaguo la kwanza la Hudgson, Kompany na Coleman lilivyokuwa kwenye kura za kuchagua mchezaji bora wa dunia, hapa ndipo maswali mengi kichwani yananijia na kunifanya niwaze hivi Mascherano, Courtois na Bale kweli ni wachezaji bora kuliko Ronaldo na Messi katika dunia ya sasa ya mpira wa miguu?.

Na baada ya kupitia matokeo mazima ya upigaji kura wa tuzo za Ballon d’Or kwa mwaka 2014 ndipo nlipogundua kwamba upigaji wa kura za tuzo hiyo umejaa urafiki, unafki mwingi na pia utaifa kuliko uhalisia. 

Sikatai kwamba upigaji kura ni maoni binafsi ya makocha na manahodha wa timu mbalimbali za taifa pia waandishi maalum wa habari. Lakini ukiangalia jinsi upigaji huo wa kura unavyofanyika ndipo unapogundua kwamba unakosa uhalisia wa kwamba mchezaji bora ni yupi hasa duniani na kwa vigezo gani?

Hebu tuangalie mifano michache ya jinsi upigaji huu wa kura ulivyoenda hasa kwa chaguo la kwanza ambalo lina pointi tano kwenye uhesabuji wa kura, kocha wa Brazili Carlos Dunga chaguo lake la kwanza alikuwa ni Neymar, kocha Wales Chris Coleman chaguo lake la kwanza ni Bale.

Kocha wa Ujerumani Joachim Low ni Manuel Neuer, kocha wa Uholanzi Guus Hiddink ni Arjen Robben, kocha wa Marekani ambaye ni Mjerumani chaguo lake la kwanza ni Manuel Neuer na kocha wa Colombia chaguo lake la kwanza ni James Rodriguez.

Kwa mifano hiyo michache ya jinsi makocha wa timu mbalimbali za taifa walivyopiga kura hasa kwa chaguo la kwanza utaona kabisa wengi wao waliweka utaifa mbele kuliko uhalisia wa kwamba mchezaji yupi ni bora duniani hasa ukijiuliza kivipi wachezaji hao ni bora mbele ya Ronaldo na Messi?

Kwa upande wa kura za manahodha kilichoangaliwa zaidi ni utaifa na urafiki ili kulinda uhusiano kati ya mchezaji mmoja na mwingine kuliko uhalisia wenyewe kwamba nani anastahili kunyakua tuzo ya mcheaji bora duniani.

Ronaldo ambaye ni mshindi chaguo lake la kwanzakwenye kura ni Sergio Ramos ambaye wanacheza wote klabu ya Real Madrid, Messi alimpa kura yake Angel di Maria ambaye wanatoka wote Argentina, Radamel Falcao alimpa James Rodriguez ambaye wanatoka wote Colombia, Diego Godin alimpa Diego Costa ambaye alikuwa mchezaji mwenzake Atletico Madrid.
 
Bastian Schweinsteiger aliwapigia kura wachezaji wa tatu anaotoka nao Ujerumani ambao ni Neuer, Lahm na Muller, Ashley William chaguo lake la kwanza ni Gareth Bale ambaye wanatoka wote Wales na Robin van Persie chgauo la kwanza ni Arjen Robben ambaye wanatoka wote Uholanzi.

Mchezaji ambaye alionyesha unafki ni nahodha wa timu ya taifa ya Poland na mshambuliaji wa Bayern Munich, Robert Lewandoski, mshambuliaji huyo baada ya Ronaldo kutangazwa mshindi aliibuka na kusema kama angepewa nafasi ya kupiga kura kwa mara nyingine basi kura yake angempa Manuel Neuer ambaye wanacheza wote klabu ya Bayern Munic.

Swali la kujiuliza ni kwamba inamaana Lewandoski hakujua kama alitakiwa kumpigia Neuer mwanzoni kabisa na kuamua kumpigia kura Ronaldo? Ama anaona aibu kuukubali ukweli kwamba Ronaldo alistahili kushinda tuzo hiyo na pia inawezekana (unafki wenyewe) labda anataka kumpoza Neuer.

Hivyo ndivyo upigaji kura wa kura ulivyokuwa kwa sehemu kubwa ya mchakato mzima wa kutafuta mchezaji bora wa dunia kwahiyo usishangae ukiambiwa Mascherano ama Paul Pogba ni wachezaji bora duniani kuliko Ronaldo na Messi.
NAWASILISHA.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!