Searching...
Image and video hosting by TinyPic
6 January 2015
Tuesday, January 06, 2015

MAKALA: AFCON YA WAZUNGU INAYOCHEZWA AFRIKA.


Na Chikoti Cico


Michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika yaani AFCON kwa mwaka 2015 itaaanza kushika kasi Januari 17 nchini Equatorial Guinea mpaka Februari 8 mwaka huu.

Michuano hiyo itazishirikisha timu 16 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika yaliyoweza kufuzu kuingia kwenye michuano hiyo mikubwa.

Katika historia ya soka barani Afrika AFCON ni michuano yenye heshima kubwa huku ikiwa sehemu ya utambulisho wa tamaduni za kiafrika kutoka nchi mbalimbali zinazoshiriki lakini pia ni michuano ambayo huzileta nchi za kiafrika karibu katika mambo ya kidiplomasia na mahusiano.

Pamoja na kuwa michuano hii ni ya Afrika lakini ukiangalia makocha wa timu shirikishi kwa mwaka 2015 ni kama vile michuano hii ni ya wazungu lakini inafanyika barani Afrika hasa baada ya makocha wa kizungu kutawala katika kuzifundisha timu hizo.

Kuelekea michuano ya AFCON 2015 makocha wa kiafrika watakaofundisha kwenye michuano hiyo ni kutoka nchi tatu tu ambazo ni Afrika ya Kusini (Ephraim Mashab), Zambia (Honour Janza) na Jamhuri ya watu wa Kongo (Florent Ibenge).

Timu zitakazofundishwa na makocha wa kigeni ni Algeria (Christian Gourcuff) Senegal, (Alain Giresse) Ivory Coast (Herve Renard) Guinea (Michel Dussuyer) na Congo (Claude Le Roy) ambao makocha wote hao wanatoka nchini Ufaransa.

Pia Tunisia (Georges Leekens) na Burkina Faso (Paul Put) ambao makocha wao wanatoka nchini Ubelgiji, Cape Verde (Rui Aguas) na Gabon (Jorge Costa) makocha wao wanatoka nchini Ureno, wengine ni kutoka Ujerumani (Kameruni, Volker Finke), Poland (Mali, Henryk Kasperczak), Israeli (Ghana, Avram Grant) na Argentina (Equatorial Guinea, Esteban Becker).

Sina ajenda ya siri dhidi ya makocha wa kigeni kwasababu hata timu za mataifa kutoka nchi nyingine nje ya bara la Afrika zimekuwa zikifundishwa na makocha wa kigeni lakini kinachonipa mgagaziko ni kuona makocha wa kiafrika wakibaki kuwa wasaidizi ama watafsiri na sio makocha wakuu wan nchi zao.

Ukiangalia tokea kuanzishwa kwa michuano ya AFCON mwaka 1957 makocha wa kigeni walioweza kunyakua kombe hilo ni 14 huku makocha wa kiafrika wakiwa ni 15 hii ikionyesha dhahiri kwamba tofauti ya makocha wa kigeni na makocha wa kiafrika ni ndogo.

Mfano mzuri ni kutoka nchini Misri ambapo kwenye michuano ya AFCON kwa mwaka 2010 waliweka rekodi mpya ya kuwa timu ya kwanza kuchukua kombe hilo mara tatu mfululizo huku mara zote hizo hizo wakiongozwa na kocha mzawa Hassan Shehata.

Na kwenye historia ya michuano hiyo Misri wamechukua kombe hilo mara saba huku mara tano kati ya hizo wakiongozwa na makocha wazawa pia nchi ya Ghana wamechukua kombe hilo mara nne na mara zote hizo timu hiyo maarufu kama “Black Stars” ilikuwa chini ya makocha wazawa.

Lakini kwa upande mwingine inawezekana chanzo cha makocha wazawa kutokupewa nafasi ni “mentality” ya viongozi wa soka la Afrika ambao wanaamini makocha wa kigeni ni bora zaidi kuliko makocha wazawa.

Na pia mara zote ambazo makocha wazawa wamekuwa wakipewa kuzifundisha timu za taifa barani Afrika wamekuwa hawapewi “support” ya kutosha wala “motivation” yoyote zaidi ya kufanyiwa fitna na kubezwa hivyo mwishowe kuonekana kwamba hawafai kuzifundisha timu hizo.

Mfano mzuri wa kukosekana kwa motisha kwa makocha wazawa ni katika listi ya mishahara ya makocha 32 kwenye michuano ya kombe la Dunia iliyofanyika nchini Brazili mapema mwezi Julai mwaka 2014 ambapo makocha wazawa walikuwa wakipokea mishahara midogo zaidi ukilinganisha na makocha wa kigeni.

Kocha wa Nigeria, Stephen Keshi alishika na nafasi ya 28 kwenye listi hiyo akichukua mshahara wa kiasi cha dola 392,420 na aliyekuwa kocha wa Ghana, James Kwasi Appiah alishika nafasi ya 31 akichukua mshahara wa kiasi cha dola 251,770.

Huku aliyekuwa kocha wa Ivory Coast, Sabri Lamouchi kutokea nchini Ufaransa akishika nafasi ya 18 na kuchukua mshahara wa kiasi cha dola 1,037,450, mshahara ambao ni zaidi ya mara nne ya mshahara wa aliyekuwa kocha wa Ghana James Appiah.

Nawaza katika mazingira kama hayo ni kocha yupi mzawa atavutika kuzifundisha timu za taifa barani Afrika.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!