Searching...
Image and video hosting by TinyPic
8 January 2015
Thursday, January 08, 2015

Hiki ndicho kilichowaponza Yanga kwa JKU.


 Na Samuel Samuel

Hatimaye uchu na kiu ya wana Jangwani kushuhudia timu yao ikipata ushindi na kutinga kwenye hatua ya Nusu Fainali ya mashindano ya Mapinduzi Cup, imeingia dosari baada ya timu hiyo kufungwa kwenye mchezo wa robo fainali na timu ya JKU ya Zanzibar bao 1-0.

Mabingwa hao wa kihistoria wa ligi kuu Tanzania bara, walikuwa tayari wameteka hisia za wapenzi wa mchezo wa soka kufuatia kucheza soka safi huku wakitoa vipigo kwa kwenda mbele kwa kila timu waliyokutana nayo kwenye hatua ya makundi bila kuruhusu nyavu zao kuguswa.

Moja kati ya sabau ya timu hiyo kuondolewa, hofu ilikuwa kubwa kuliko uhalisia. Namkubali sana kocha wa Yanga, Hans Pluijm lakini leo kuna kitu kanishangaza kidogo. 

Ukiwatazama JKU wana uwezo mkubwa hasa katika nafasi ya kiungo na ulinzi. Toka mechi za awali wameonesha uwezo mkubwa kwenye kiungo cha chini na juu. 

Kama utakuwa makini, utagundua kuwa kocha Hans aliamua kujilinda zaidi kwenye mchezo huo wa robo fainali kuliko kushambulia kama ilivyo kawaida yake. 

Amemtumia Salum Telela kama kiungo mkabaji chini lakini akamuanzisha pia Hassan Dilunga mbele ambaye naye kiasilia ni mkabaji. Unapowaanzisha wachezaji wa aina moja kwenye kiungo, unapoteza mtu wa kuichezesha timu.

Kwa sababu hiyo ndiyo maana utaona sehemu yote ya kati timu ilijiandaa kuzuia zaidi na kuharibu mipangoe ya adui kuliko kutengeneza muunganiko wa timu. 

Bado sifahamu ni kwa nini mechi kama hii benchi la ufundi wameshindwa kumuanzisha Haruna Niyonzima. Ukiwa na Haruna ni rahisi kuwahadaa timu pinzani kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira na kutengeneza nafasi huka akiachia pasi za uhakika.

Mshambuliaji Kpah Sherman hakuwa kwenye kiwango bora baada ya kukosa nafasi nyingi za wazi na katika hili, ni lazima kocha msaidizi Boniface Mkwasa na bosi wake, Hans Van Der Pluijm waongeze ukali kidogo.

Unapotumika kama mshambuliaji namba mbili ni lazima ujifunze kutawanya mipira kwa wakati na kujaribu kukunjua miguu yako kuelekea goli la adui. Ni lazima apambane kama mshambuliaji Hamisi Kiiza alivyokuwa anakunjuka akiwa karibu na goli. 

Pamoja na makosa hayo, bado Yanga pia ilionekana kama timu ambayo haikuwa na bahati. Nafasi ambazo zilipatikana, zilitosha kuwapeleka wana Jangwani hatua inayofuata lakini hazikutumika sawa sawa.

Kuna uwezekano wachezaji wa Yanga waliingia dimbani huku wakiwa na uhakika wa kuwafunga JKU magoli mengi tu kutokana na timu hiyo kuonekana chini ya kiwango ukilinganisha na Yanga.

Matokeo yake wakajikuta wanapoteza umakini na kutumia nafasi kadhaa zilizotengenezwa kupitia Simoni Msuva na Andrey Coutinho.

Ni lazima pia kuwapongeza JKU kwa ushindi waliopata kwani walionekana kucheza vizuri huku wakiiheshimu timu ya Yanga kitu ambacho kimewasaidia kuweza kuibuka na ushindi. 

Kwa matokeo hayo basi, JKU watacheza na Mtibwa Sugar huku Wekundu wa Msimbazi, Simba Sc wakikutana na Polis Zanzibar kwenye michezo ya hatua ya nusu Fainali.


0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!