Na Chikoti Cico
Tarehe 18 ya mwezi Agasti 2014 ndipo pazia la ligi kuu nchini Uingereza lilifunguliwa na moja ya mechi ilikuwa ni Burnley dhidi ya Chelsea, mchezo ulioisha kwa Chelsea kushinda kwa magoli 3-. l
kilichovutia mashabiki wengi kwenye mchezo huo ni jinsi goli la pili la Chelsea kwenye dakika ya 21 lililovyofungwa na mshambuliaji wa kijerumani wa Chelsea, Andre Schurrle.
Goli hilo lilitokea baada timu ya Chelsea kupiga pasi zaidi ya 20 kabla ya pasi ya Cesc Fabregas iliyopigwa katikati ya mabeki wa Burnley kumfikia Schurrle aliyeipatia Chelsea goli la pili.
Ubora wa pasi za Chelsea mpaka goli hilo kufungwa ulikuwa wa hali ya juu, na timu iliyokuwa inajulikana kama “wapaki basi” sasa ikaanza kuitwa “Barcelona ya blue” na hasa baada ya kupiga pasi 751 kwenye mchezo mwingine uliofuatia dhidi ya Crystal Palace ambapo Chelsea ilishinda kwa magoli 2-1.
Huku sehemu kubwa ya ubora wa pasi hizo ukichangiwa na Fabregas aliyesajiliwa na Chelsea kutoka Barcelona.
Na mpaka mzunguko wa kwanza wa ligi kuu nchini Uingereza unafikia tamati Chelsea walikuwa wamepoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Newcastle United na kutoka sare michezo minne huku wakishinda michezo 14.
Ubora wa pasi za Chelsea na ushindi kwenye mechi nyingi za mzunguko wa kwanza. ulifunika makosa ya waamuzi na mbinu chafu za timu pinzani kwenye macho ya Mourinho.
Lakini baada ya mchezo dhidi ya Newcastle ndipo kocha huyo akaanza kuionyesha dunia kwamba Chelsea inaonewa na ni timu bora isiyokosea bali waamuzi na mbinu chafu kutoka kwa timu pinzani ndizo husababisha Chelsea kutokushinda mechi.
Hebu tuangalie mahojiano mbali mbali ambayo Mourinho alifanya kila baada ya mechi ambazo hakupendezwa na matokeo yalivyokuwa tokea mzunguko wa kwanza na mechi ya kwanza ya mzunguko wa pili.
Baada ya mchezo dhidi ya Newcastle ambapo Chelsea walifungwa kwa magoli 2-1 Mourinho alilalamikia uchelewashaji wa mpira kurushwa uwanjani akiongea na waandishi wa habari alisema,
“wakati mwingine kulikuwa hakuna mipira na hilo lilisitisha mwendelezo wa timu (Chelsea) iliyokuwa inajaribu kushinda”
Hapa Mourinho alikuwa anataka kuiambia dunia kwamba “ball boys” ndiyo sababu ya Chelsea kushindwa kurejesha magoli yote mawili na hata kushindwa mchezo huo.
Lakini kocha huyo hakuzungumzia ubora wa magoli ya Newcastle na makosa ya mabeki wake yaliyosababisha Papiss Cisse kufunga magoli yote mawili, bado alitaka kutuonyesha kwamba Chelsea huwa hawakosei.
Kwenye mechi nyingine ya mwisho wa mzunguko wa kwanza wa ligi ya Uingereza dhidi ya Southampton mchezo ulioisha kwa sare ya goli 1-1 Mourinho akihojiwa na waandishi wa habari hakuzungumzia kabisa kosa la Terry lililozaa goli la Southampton wala ubora wa timu ya Southampton kwenye kipindi cha kwanza zaidi alihamishia makosa kwa mwamuzi wa mchezo huo Anthony Taylor.
Alikaririwa na vyombo vya habari akisema “ kuna kampeni (ya kuinyima Chelsea penati) dhidi ya Chelsea sijui kwanini kuna kampeni na sijali, kila mtu anajua ilikuwa ni penati.
Mwamuzi alifanya kosa, watu wanafanya makosa na alifanya kosa” Ingawa tukio la Chelsea kunyimwa penati kwenye mchezo huo lilikuwa ni kweli lakini Mourinho bado aliendelea kuifanya Chelsea ionekane haikustahili kutoa sare na Southampton hata kwa kosa la wazi toka kwa John Terry.
Baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi hatimaye mzunguko wa pili ulianza huku Chelsea ikicheza dhidi ya Tottenham Hotspur mchezo ulioisha kwa Chelsea kufungwa kwa magoli 5-3.
Baada ya mchezo huo Mourinho alielekeza lawama zake kwa mwamuzi Phil Dowd kwa kuinyima Chelsea penati kwenye kipindi cha kwanza lakini Mourinho wala hakujaribu kusema chochote kuhusu ubovu ulioonyeshwa na beki ya Chelsea kuruhusu magoli matano huku mshambuliaji wa Spurs Harry Kane akiinyanyasa beki hiyo atakavyo.
Mourinho alisema “ninashtushwa na mambo mengine kuliko kufungwa magoli matano, ninashtushwa kwamba ndani ya siku tatu tumekuwa na maamuzi mawili ya kushangaza ambao yalituadhibu katika namna mbaya sana”
Mourinho akionyesha kugadhabika kwa maamuzi ya mwamuzi huyo aliendelea kusema “matokeo yakiwa 1-0 tendo moja lililo wazi lingeweza kufanya iwe 2-0, matokeo na historia ya mchezo ingekuwa tofauti, meneja na wachezaji tunashinda na kupoteza lakini Mr Dowd hakupoteza, huu ni uamuzi ambao ni ngumu kuukubali”
Huyo ndiye Jose Mourinho ambaye mara zote huwatupia lawama watu wengine hata kwa makosa ya wazi yanayoonekana kwa timu yake, huku ikiwa ni njia rahisi ya kuitoa presha kwa wachezaji wake katika kutafuta ubingwa na kuipeleka presha hiyo kwa waamuzi lakini huyo ndiye Mourinho na sitashangaa waamuzi wakaanza kuipa Chelsea penati kwa mechi zinazokuja.
0 comments:
Post a Comment