Barcelona wachapwa na David Moyes.
Na Oscar Oscar Jr
Leo imekuwa siku mbaya kwa timu kubwa za nchini Hispania baada ya kujikuta zikichezea vipigo ugenini kwenye mechi za La Liga ambazo zimerejea kwenye viwanja mbalimbali.
Real Madrid mapema walifungwa na Valencia kwa bao 2-1 na mchezo wa usiku, umeshuhudia Barcelona wakipoteza mchezo mbele ya Real Sociedad kwa bao 1-0 ambalo Jordi Alba amejifunga huku Lionel Messi na Neymar wakianzia benchi.
Timu hiyo ambayo kwa sasa inaongozwa na aliyekuwa kocha wa Manchester United, David Moyes msimu huu itakuwa imewapa furaha sana mashabiki wake baada ya kuzichapa timu tatu za juu kwenye msimamo wa La Liga.
Sociedad walianza na Atletico Madrid, kisha wakawachapa Real madrid na leo wamehitimisha kwa timu ya Barcelona. David Moyes amefanikiwa kulinda rekodi ya Real Sociedad ya kutofungwa nyumbani kwenye La Liga na Barcelona tangu mwaka 2008.
Sociedad ambao walikuwa na shuti moja tu lililolenga lango huku wakiwa na umiliki wa mpira kwa asimilia 27, wamefanikiwa kuongeza pointi tatu muhimu na sasa wamefikisha alama 18 na kupanda kwenye msimamo wa ligi hiyo hadi nafasi ya 13.
Kutokana na kichapo hicho, Barcelona wanaendelea kusalia na alama zao 38 ambazo ni sawa na walizopata Atletico Madrid baada ya ushindi wao wa mchezo uliopita, huku Real Madrid pamoja na kichapo cha bao 2-1 walichopata bado wanabakia kileleni wakiwa na alama 39 na mchezo mmoja pungufu.
0 comments:
Post a Comment