Torres apokelewa Kifalme.
Na Oscar Oscar Jr
Katika hali ya kushangaza hivi karibuni Mshambuliaji ambaye ameonekana kuchokwa na Mashabiki wa Chelsea na wale wa Ac Millan, Fernando Torres aliamua kurudi nyumbani kujiunga na timu yake ya utotoni Atletico Madrid, alikaribishwa na mashabiki 40,000 kwenye dimba la Vicente Calderón.
Torres ambaye amekipiga na Ac Millan huku akiwa amefunga bao moja tu kwenye mechi 10 huko nchini Italia, ameamua kurudi kwenye klabu yake iliyomkuza ambayo aliachana nayo tangu mwaka 2007 alipojiunga na Liverpool na mapokezi aliyopewa ni kama ya Kifalme.
Fernando Torres alikuwepo Jukwaani wakati timu yake akipata ushindi dhidi ya Levante na sasa anatajwa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza kitakachocheza na Real Madrid kwenye mchezo wa Kombe la Mfalme siku ya Jumatano.
Torres ambaye aliingia na watoto wake wawili huku akiwa na jezi namba 19, ameonyesha kuwagonga nyoyo mashabiki wa timu hiyo pamoja na viongozi huku Rais wa klabu hiyo, Enrique Cerezo akisema kuwa walikuwa wanamsubiria Torres tangu mwaka 2007 alioondoka na kujiunga na Liverpool na kuwafanyia makubwa kabla ya kwenda kuchemsha akiwa na Chelsea.
Hii ni isharatosha kuwa, unaweza ukaonekana kimeo ugenini lakini unapopata fursa ya kurudi nyumbani, watu wanakupa faraja ambayo umeikosa kwa muda mrefu.
Kwa sasa kazi imebakia kwa Fernando Torres kuweza kuwalipa mashabiki hao kwa kuhakikisha Atletico Madrid wanafanya vizuri.
0 comments:
Post a Comment