Na Chikoti Cico
Katika mfululizo wa mechi za ligi kuu nchini Uingereza kwenye uwanja wa The Hawathorns timu ya West Bromwich Albion itaikaribisha Manchester City.
West Bromwich Albion wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya QPR kwa kufungwa kwa magoli 3-2 matokeo yaliyopelekea timu hiyo kushika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 17.
Kocha wa West Brom Alan Irvine kuelekea mchezo atamkosa mshambuliaji wake Victor Anichebe ambaye ni majeruhi huku Graham Dorrans na Boaz Myhill ambao pamoja na kukosa mazoezi siku ya Jumanne wanatarajiwa kuwepo kwenye mchezo dhidi ya City.
Nahodha wa timu hiyo Chris Brunt ambaye alikosekana kwenye mchezo uliopita dhidi ya QPR anatarajiwa kurejea kikosini dhidi ya City sambamba na mshambuliaji Georgios Samaras ambaye amerejea kutoka Ugiriki alikokwenda kwaajili ya mambo ya kifamilia.
Kueleka mchezo huo takwimu zinaonyesha West Brom wana rekodi mbaya kwenye mechi za siku ya “Boxing day” kwani katika michezo nane iliyopita wameshinda mchezo mmoja tu huku wakifungwa michezo mitano na kutoka sare michezo miwili.
Kikosi cha kocha Alan Irvine kinaweza kuwa hivi: Foster, Wisdom, McAuley, Lescott, Pocognoli, Morrison, Brunt, Dorrans, Sessegnon, Ideye, Berahino
Manchester City wakiwa na rekodi nzuri ya kushinda michezo sita iliyopita huku wakipoteza mchezo mmoja tu ugenini wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo kutafuta alama tatu muhimu ili kuendelea kuikimbiza kileleni timu ya Chelsea ambayo inaongoza ligi ikiwa na alama 42, mpaka sasa City wanashika nafasi ya pili wakiwa na alama 39.
Kocha wa Manchester City Manuel Pellegrini bado ataendelea kuwakosa washambuliaji wake wa tatu Sergio Aguero, Edin Dzeko na Stevan Jovetic ambao ni majeruhi pia atamkosa beki wake mahiri Vicent Kompany ambaye nae pia ni majeruhi.
Kuelekea mchezo huo Manchester City wanaonekana kuwa na rekodi nzuri dhidi ya West Brom kwani katika michezo tisa iliyopita ya ligi dhidi yao wameshinda michezo nane na kutoka sare mchezo mmoja tu bila ya kupoteza mchezo wowote.
Kikosi cha kocha Manuel Pellegrini kinaweza kuwa hivi: Hart, Zabaleta, Demichelis, Kolarov, Toure, Clichy, Navas, Lampard, Silva, Milner, Nasri
0 comments:
Post a Comment