Wanachama wa Simba waja na ujumbe mzito!
Na Oscar Oscar Jr
Hatimaye wanachama wa klabu ya Simba 11 ambao walikuwa wameshitakiwa kutokana na kufanya uharibifu kwenye Uwanja wa Taifa kwa kung'oa viti na kuharibuni miundo mbinu mingine ya dimba hilo mwaka jana, wamefutiwa mashitaka na leo wameachiwa huru.
Wanachama hao waliodaiwa kufanya uharibifu huo, leo hii wamefutiwa mashitaka ambayo yalieleza gharama za uharibifu waliokuwa wanatuhumiwa kufikia Milioni 21 fedha za kitanzania.
Vurugu hizo zilitokea msimu uliopita kwenye mchezo baina ya Simba na Kagera Sugar uliomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 1-1.
Akizungumza mmoja wa wanachama hao mara baada ya kufutiwa mashitaka yao, amesema kuwa tukio hilo linapaswa kuwa somo kwao na kwa watu wengine kuhakikisha kuwa miundo mbinu ya uwanja inatuzwa na watu wote.
Mwanachama huyo hakusita kuushukuru pia Uongozi wa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Mh Ismail Aden Rage kwa kuwasaidia kuwatoa nje kwa dhamana kabla ya hii leo shitaka hilo kufutwa.
Wanachama hao ambao walikaa "Sero" ya kituo cha Chang'ombe kwa wiki moja kabla ya kupewa mdhamana, wametoa wito kwa wadau wote wa soka kila mtu kuwa mlinzi wa mwenzie ili kuepusha uharibifu mwingine wa uwanja huo ambao kila mtanzania ana jukumu la kuulinda.
Simba ambayo inakamata nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi kuu baada ya kushuka dimbani mara nane na kuambulia alama tisa pekee, siku ya Ijumaa walishuka dimbani na kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar lakini msimu huu hali ilikuwa ni tulivu kabisa na hakuna uhalibifu wowote wa Miundo mbinu uliotokea.
0 comments:
Post a Comment