Kombe la Mapinduzi lawakera watu!
Na Oscar Oscar Jr
Ndicho ambacho unachoweza kuzungumza baada ya timu zinazoshiriki ligi kuu ya Tanzania bara, Azam, Simba, Yanga na Mtibwa Sugar kupewa mualiko wa kushiriki michuano ya Mapinduzi ambayo inatarajia kuanza kutimua vumbi hivi karibuni na timu hizo tayari zimethibitisha ushiriki wao.
Moja kati ya athiri zitakazopatikana kwenye ligi kuu, ni kusimama kwa baadhi ya mechi. Weekend hii ratiba inaonyesha Azam walitakiwa kuwaalika Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Azam Complex.
Hii ni mechi ambayo wengi wangependa kuitazama hasa ikizingatiwa kuwa, Mtibwa wanaongoza ligi hiyo wakiwa na alama 16 huku Azam wao wakiwa na alama 14.
Baada ya kuonekana kama Mbeya City wanataka kurudi kwenye ubora wao baada ya kupata ushindi wao wa pili msimu huu baada ya kuifunga Ndanda Fc bao 1-0, weekend hii walitakiwa kuwakaribisha watoto wa Jangwani, timu ya Yanga kwenye dimba la Sokoine Jijini Mbeya ambako msimu uliopita timu hizo ziliweza kutoka sare ya kufungana bao 1-1.
Kwa upande mwingine, baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar, wekundu wa Msimbazi ambao wanadaiwa kuvunja mkataba na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Phiri wangekuwa na safari ya kuelekea Jijini Tanga kwenda kupambana na Mgambo JKT ambao msimu uliopita waliweza kuichapa timu hiyo kutoka mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Kocha mkuu wa Ruvu Shooting, Tom Olaba ambaye wiki iliyopita ametoka kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya watani zao timu ya JKT Ruvu, ameibuka na kusema kuwa ratiba ya Kombe la Mapinduzi itarudisha nyuma moto ambao wamekwisha uwasha.
Olaba amesema kuwa, kama ligi itasimama ni wazi kuwa wachezaji watalazimika kuvunja kambi na kurudi majumbani. Ligi itakaporejea tena, itakuwa wao kama wanaanza upya.
0 comments:
Post a Comment