Azam vs El- Merreikh kuchezwa Zanzibar
Na Oscar Oscar Jr
Azam ni timu ya tatu kuthibitisha ushiriki wao kwenye michuano ya Mapinduzi ambayo itaanza hivi karibu kule visiwani Zanzibar kutoka Tanzania bara ambapo Simba na Yanga tayari wameshathibitisha ushiriki wao.
Kupitia kwa mtendaji mkuu wa timu hiyo ambayo inakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu wakiwa na alama 14, Sad Kawemba amesema timu itashiriki na watapeleka kikosi cha kwanza.
Akizungumza kwa njia ya simu na mtangazaji wa kituo cha Redio cha E-FM, Kawemba amesema hiyo ni nafasi nyingine kwa timu yake kuweza kujiandaa na mechi za kimataifa hasa ukizingatia kuwa timu hiyo itashiriki michuano ya klabu bingwa Afrika kwa mara ya kwanza.
Moja ya maswali aliyoulizwa ni kuhusu kualikwa kwenye michuano hiyo kwa klabu ya Sudan, El-Merreikh ambayo wamepangwa kukutana nayo kwenye hatua za awali za michuano ya klabu bingwa Afrika.
Sad amesema wao hawana habari kama El- Merreikh nao wamepewa mualiko kwenye michuano hiyo lakini hakusita kusema kuwa kama nao watakuwepo, itakuwa ni vizuri kwa timu hizo kupata nafasi ya kujuana zaidi.
Timu hizo zilikutana mwaka huu kwenye michuano ya Kagame kule nchini Rwanda na kufanikiwa kutoka sare ndani ya dakika 90 za mchezo kabla ya Azam kuondoshwa kwa mikwaju ya penati.
Endapo mualiko wa El-Merreikh utathibitishwa, kuna uwezekano wadau na wapenzi wa soka wakapata mechi ya Azam vs El-Merreikh visiwani Zanzibar kupitia Mapinduzi Cup kabla ya mpambano wa klabu bingwa Afrika.
Kwa makundi ambayo yameshapangwa mpaka sasa, timu ya El-Merreikh haijajumuishwa labda kama wanaweza kupangwa kabla michuano hiyo kuanza kutimua vumbi.
0 comments:
Post a Comment