Searching...
Image and video hosting by TinyPic
30 November 2014
Sunday, November 30, 2014

Manchester United, Liverpool na Arsenal zang’ara.



Na Chikoti Cico

Ligi ya Uingereza ikiendelea kushika kasi kwenye viwanja mbalimbali siku ya Jumamosi ilishuhudia vigogo wa ligi hiyo waking’ara kwa kupata ushindi katika mechi mbalimbali hivyo kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi kuu nchini Uingereza.

Kwenye uwanja wa Old Trafford Manchester United waliibuka kidedea kwa kuifunga timu ya Hull City kwa magoli 3-0, magoli ya United yalifungwa na Chris Smalling dakika ya 16, Wayne Rooney dakika ya 42 kabla ya Robin Van Perse kuihakikishia United alama tatu muhimu kwa kufunga goli la tatu kwenye dakika ya 66 ya mchezo huo.

United walitawala sehemu kubwa ya mchezo na kwa ushindi huo wamebaki nafasi ya nne wakiwa na alama 22 ingawa walimpoteza kiungo wao mwenye kasi Angel Di Maria ambaye aliumia na kutolewa nje kwenye dakika ya 14 ya mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na Herrera.

Kwenye uwanja wa Hawthorns ambako West Bromwich waliikaribisha timu ya Arsenal, mchezo ulimalizika kwa Arsenal kupata ushindi mwembamba wa goli 1-0 goli lililofungwa na Danny Welbeck kwenye dakika ya 60 ya mchezo huo.

Wakati huo huo baadhi ya mashabiki wa Arsenal walibeba bango lenye kutaka kocha wa timu hiyo Arsene Wenger kuondoka maandishi hayo yalisomeka “Arsene asante kwa kumbukumbu ila ni muda wa kusema kwaheri”

Katika mchezo huo wachezaji wa Arsenal waliokuwa majeruhi kama Olivier Giroud na beki Laurent Koscielny walirejea kikosini baada ya kuwa nje kwa muda mrefu, ushindi huo wa Arsenal umewasogeza mpaka nafasi ya sita wakiwa na alama 20.

Vigogo wengine wa ligi kuu nchini Uingereza waliopata ushindi baada ya kuwa na mfululizo wa matokeo mabovu ni timu ya Liverpool.

Wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani Anfield timu ya Liverpool ilipata ushindi mwembamba wa goli 1-0 dhidi ya Stoke City kwa goli lilifungwa na beki wa kulia Glen Johnson kwenye dakika ya 85 ya mchezo.

Ushindi huo wa Liverpool utakuwa umepunguza presha kidogo kwa kocha Brendan Rodgers ambaye mpaka sasa amekalia kuti kavu baada ya kuwa na matokeo ya kutokuridhisha kwa mechi za karibuni, kwa ushindi huo Liverpool wameshika nafasi ya 11 wakiwa na alama 17 sawasawa na Spurs na Everton ambao wanacheza leo.

Pia katika mchezo huo Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard aliyeingia dakika ya 75 alifikisha miaka 16 ya kuvaa jezi za timu hiyo toka mara ya kwanza kabisa alipotokea benchi na kuichezea Liverpool kwenye uwanja wa Anfield.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!