Na Chikoti Cico
Ligi kuu ya Uingereza itaendelea tena wikendi hii na moja ya mechi inayosubiriwa kwa hamu, ni kati ya Manchester United dhidi ya Chelsea, mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Old Trafford majira ya saa moja kamili jioni siku ya Jumapili.
Huu ni mchezo ambao utawakutanisha makocha Luis Van Gaal na Jose Mourinho ambao kwa pamoja waliwahi kuifundisha timu ya Barcelona huku Van Gaal akiwa kocha mkuu na Mourinho akiwa kocha msaidizi wa tatu.
Kocha wa Manchester United Luis Van Gaal anatarajiwa kuingia kwenye mechi hii kutafuta alama tatu muhimu dhidi ya vinara Chelsea na kuweza kupunguza tofauti ya alama 10 iliyopo sasa kwenye msimamo wa ligi.
Mpaka sasa Manchester United wanashika nafasi ya sita huku wakiwa na alama 12 wakati Chelsea, wanashikilia usukani wa ligi wakiwa na alama 22.
Kiungo Angel Di Maria ambaye aliumia kwenye mechi dhidi ya West Bromwich Albion anatarajiwa kuwa fiti kuikabili Chelsea wakati huo huo, Manchester United itaendelea kumkosa mshambuliaji Mwingereza Wayne Rooney ambaye bado anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu baada ya kupewa kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya West Ham na huu utakuwa mchezo wake wa mwisho kuukosa.
Kikosi cha Manchester United kinaweza kuwa hivi: De Gea; Rafael, Jones, Rojo, Shaw; Blind, Herrera, Mata, Di Maria; Falcao, Van Persie
Vinara wa ligi kuu ya Uingereza Chelsea wataingia kwenye mtanange huo wakitaka kuendeleza rekodi yao nzuri ya kutofungwa hata mechi moja mpaka sasa kati ya mechi nane za ligi walizocheza.
Pia kuendeleza rekodi nzuri ya mechi za ugenini ambapo mpaka sasa imecheza michezo minne na kushinda michezo mitatu na kutoka sare mchezo mmoja.
Kocha wa Chelsea Jose Mourinho anaweza kuwakosa washambuliaji Diego Costa na Loic Remy ambao ni majeruhi ingawa alipohojiwa na waandishi wa habari, alisema “kuna uwezekano wa Costa kuweza kucheza”
Viungo John Obi Mikel na Ramirez ambao ni majeruhi, nao wana hatihati ya kutokucheza mchezo huo siku ya Jumapili huku beki wa kushoto Filipe Luis, akitarajiwa kuanza kuchukua nafasi ya Cesar Azpilicueta aliyepewa kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya Crystal Palace.
Kikosi cha Chelsea kinaweza kuwa hivi: Courtois; Ivanovic, Cahill, Terry, Luis; Matic, Fabregas; Willian, Oscar, Hazard; Drogba
Takwimu zinaonyesha Manchester United wamefunga magoli 15 na kufungwa magoli 12, huku Chelsea wakifunga magoli 23 na kufungwa magoli nane mpaka sasa toka msimu wa ligi kuanza.
0 comments:
Post a Comment