Uchambuzi: Azam wageuka wababe wa Mbeya City.
Na Oscar Oscar Jr
Katika mechi tatu ambazo Mbeya City wamekutana na Azam, timu ya Azam imejikusanyia alama saba huku Mbeya City wakiambulia pointi moja pekee.
Sifa moja ya timu inayohitaji ubingwa, ni kupata matokeo mazuri bila kujali kama wamecheza vizuri au vibaya. Jana Azam ameshinda bao 1-0 dhidi ya Mbeya City.
Azam jana hawakucheza mchezo ambao mtazamaji angependa kuushuhudia lakini, walikuwa na ile ya sifa ya timu inayohitaji ubingwa.
Kupata matokeo mazuri bila kujali aina ya soka walilocheza na wakafanikiwa. Mbeya City wameendelea kuwa wanyonge wanapocheza Sokoine dhidi dhidi ya Azam na hilo halina ubishi. Azam ndiyo timu pekee ya ligi kuu kushinda mechi zake pale Sokoine dhidi ya Mbeya City.
Mbeya City wamekuja zama ambazo Azam wanaonekana kuwa kwenye ubora wa juu pengine kuliko msimu wowote tangu waingie ligi kuu. Kitendo cha kucheza michezo zaidi ya 30 ya ligi kuu bila kupoteza, kitendo cha timu hiyo kuwa na safu bora ya ulinzi msimu uliopita, na kutwaa ubingwa wao kwa mara ya kwanza, inathibitisha ubora wao.
Tatizo kubwa kwa Mbeya City, bado lipo kwenye safu yao ya ushambuliaji. Pamoja na kuwa na wachezaji kama Poul Nonga, Themi Felix, Saad Kipanga na mtu mzima Mwagane Yeya, mpaka sasa wamefunga bao moja tena kupitia mkwaju wa Penati.
Michezo pekee timu hiyo ilipoonyesha ubora wa safu yao ya ushambuliaji, ilikuwa pale Azam Complex msimu uliopita walipotoka sare ya kufungana 3-3 dhidi ya Azam na sare ya 2-2 dhidi ya Simba pale uwanja wa Taifa.
Jina la Mwagane Yeya ni kubwa kuliko idadi yake ya magoli, alifunga magoli matano tu msimu uliopita tena manne kati ya hayo akiyafunga dhidi ya timu moja (Azam) kwenye michezo miwili waliyokutana.
Ukitazama kikosi cha kocha Juma Mwambusi kinavyoanza, huwa na washambuliaji zaidi ya watatu. Nadhani huu ni muda muafaka wa kulitazama suala hili kwa sababu, timu inaonekana kuanza na washambuliaji wengi kuliko viungo wachezeshaji.
Viungo wengi wa Mbeya City ni defensive minded kitu kinachowafanya washambuliaji wa timu hiyo kutofunga magoli mengi.
Mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting uliomalizika kwa sare pacha, walitengeneza nafasi nyingi sana za kufunga magoli ingawa washambuliaji wao walikosa umakini na kushindwa kufunga lakini, safu ya ulinzi ya Ruvu Shooting, huwezi kuifananisha na ile ya Azam. Azam inaukuta mgumu sana, inahitaji ufundi wa hali ya juu kuifungua.
Bado Mbeya City wana nafasi ya kufanya vizuri lakini, wanapaswa kuwa na mpango B. Ile roho ya kupambana bila kujali kutanguliwa kufungwa waliyokuwa nayo msimu uliopita, inabidi irejee.
Kwa sasa Mbeya City wanakila kitu cha kuwafanya kufanya vizuri. Ni muda wa Uongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki wao kukaa pamoja na kuisapoti timu. Jana wamefungwa na timu bora.
0 comments:
Post a Comment