NANADO, BENZI NA DISKO LA SANTIAGO BERNABEU
NA MARKUS MPANGALA
KISA cha mashabiki wa Real Madrid kumchukia Luis Enrique ni kitendo cha kuihama timu hiyo kwenda Barcelona, huku akichafua hali ya hewa baina yake na mashabiki. Luis Figo naye alitimka Barca kwenda Real Madrid na kuchafua hali ya hewa baina yake na mashabiki wa Catalunya.
Luis Enrique aliendeleza vita ya maneno na viongozi wa Real Madrid pamoja na mashabiki wao.
Figo aliamua kunyamaza licha ya shutuma mbalimbali za mashabiki wa Barca na kueleza ugomvi wake na viongozi wa Barcelona tu si mashabiki. Enrique alirejea kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu wikiendi iliyopita akiwa na kikosi chake cha Barcelona.
Ikumbukwe msimu uliopita alikileta kikosi chake cha Celta Vigo, alizomewa kama ilivyo tabia ya mashabiki. Lakini Luis Enrique ndiye bosi wa Barcelona.
Amekuwa kocha mkuu baada ya kutwaa mikoba ya Tata Martino. Baada ya kuona pambano la El Clasico la kwanza chini ya Luis Enrique hakika siwezi kuihofia tena Barcelona.
Enrique hawezi hata kujaribu kile alichokuwa kikifanya Tata Martino, labda atajitetea kwamba anaanza kujenga timu mpya baada ya mastaa Xavi, Iniesta na Pique kuporomoka uwezo wao.
Pambano la wikiendi iliyopita, Enrique alianza na washambuliaji watatu hatari, Luis Suarez, Neymar na Lionel Messi. Majina na uchezaji wao ulikuwa tofauti mno uwanjani.
Messi amerudishwa nyuma kucheza namba kumi kama kiungo huru. Neymar anapangwa kushoto kama kawaida. Suarez anacheza nambari tisa akiwa na eneo dogo sana la kukimbia. Ukimwangilia Suarez yule wa Liverpool kisha ukimwona Suarez wa Barcelona.
Akiwa Barcelona anacheza kwenye eneo dogo sana na anatakiwa kusimama eneo la kushambulia pekee huku kazi kubw aikifanywa na Messi na Neymar.
Mbinu za Enrique zimeonesha namna Andres Iniesta alivyonyimwa ule uhuru wa mwanzo. Iniesta anacheza smabamba na Neymar upande wa kushoto kuelekea katikati kuungana na Xavi na Messi.
Kwa mtindo huo walijikuta wanakabiliana na Luka Modric aliyekuwa na kazi ya kuituliza timu. Xavi alijikuta akikabiliana na wachezaji wawili, Toni Kroos na James Rodriguez.
Kwa James Rodriguez alikuwa na kazi mbili, kusaidia ulinzi upande wa kulia chini-katikati, kisha Karim Benzema(Benzi) akicheza kama mshambuliaji huru mno eneo lote la lango la Barcelona.
Benzema, muite Benzi alikuwa na kazi hii kwenye mechi ya Liverpool. Yeye habanwi sana na kubaki eneo la nambari tisa kwakuwa hajapewa kazi ya kufunga pekee bali kutengeneza mabao.
Kuna wakati eneo la namba 9 linakuwa tupu, lakini mpira unakuwa mikononi mwa wachezaji wenzake wa karibu kati ya Ronaldo (Nanado) au James Rodriguez).
Uhuru aliokuwa nao Benzi uliwafanya mabeki wa Barcelona washindwe kuwa na udhibiti wa mshambuliaji kamili. Benzi aliweza kurudi katiati ya dimba kufuata mpira.
Rodriguez alirudi kusaidia ulinzi, wakati Ronaldo (Nanado) alikuwa anaiondoa timu kutoka eneo lake kwenda lango la adui kwa kasi. Mwisho kulikuwa na Isco au muite Disko.
Yeye alicheza kwa staili ya Clarence Seedorf. Kazi yake kubw ailikuwa kuwafanya washambuliaji watatu; Benzi, Nanado na James wanakuwa na pasi za uhakika eneo la adui. Kipindi cha kwanza Isco hakucheza vizuri na alipoteza mipira kirahisi mno.
Lakini kipindi cha pili alicheza vizuri na alichukua jukumu la kusaidia ulinzi upande wa kushoto chini kwa Marcelo kama alivyofanya James kwa Dani Carvajal. Disko na James walikuwa na nafasi nzuri ya kuwasaidia Nanado na Benzi hasa kutokana na umahiri wa Modric na Kroos.
Toni Kroos alikuwa na kazi ya kuwalinda mabeki wake, akisaidia na Modric. Mjerumani huyu hakika anasisimua jinsi anavyojituma na kutoa pasi za uhakika. Wale wlaiosema Real Madrid itayumba kuondokewa na Xabi Alonso watakubaliana name kuwa nilikuwa nabishia suala hilo kitaalamu jamani.
Na sasa tunamsahau Alonso, kisha tunaye Kroos ingawa halingani na Mhispania yule kwa pasi ndefu. Kitu kimoja kinachotakiwa kujulikana kwa mashabiki wa Real Madrid na wapinzani wetu ni kwamba, tuna ngome imara kwenye kiungo na ‘Blan B’. Sami Khedira ‘Mwarabu’ aliingia kuvunja vunja kiungo cha Barca kumdhibiti Sergio Busquet.
Kwa kocha huyu Luis Enrique hakika Barcelona itapata shida kwa Real Madrid na hata jirani zetu Atletico Madrid wataisumbua Barca. Haaaaaaa! Wanalo msimu huu aisee! Labda wakimbie La Liga, Catalunya ikijitenga!
0 comments:
Post a Comment