Na Oscar Oscar Jr
Ikiwa ni mechi tano tu ambazo zimechezwa kwenye ligi kuu ya Vodacom, Mtibwa Sugar wameonekana kuanza vizuri sana. Mtibwa Sugar wanaongoza ligi kuu wakiwa na alama 13 huku wakiwa wameshafunga magoli manane.
Novemba mosi, katika dimba la Jamhuri mkoani Morogoro, watakutana na timu ya Simba ambayo inaonekana kuingia mgogoro baada ya kutoka sare kwenye michezo yao mitano ya awali.
Tayari kuna taarifa za wachezaji watatu wa timu hiyo kusimamishwa ambao ni Haruna Chanongo, Amri Kiemba na Shaban Kisiga.
Mtibwa wanarejea uwanja wa nyumbani baada ya kupata ushindi ugenini dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wa Sokoine, huku washambuliaji wa timu hiyo, Ame Ally na Ally Shomary wakionekana kuwa moto wa kuotea mbali.
Kocha wa Simba, Patrick Phiri anaonekana kutokuwa na msimamo kwa sababu, kitendo cha viongozi wa Simba kuwaondoa kambini baadhi ya wachezaji na kuwatuhumu kuwa wanahujumu timu huku yeye akiendelea kukaa kimya, inaibua wasiwasi mkubwa wa taaluma yake.
Phiri amepewa mechi mbili na asiposhinda, kibarua chake kitakuwa matatani. Kitendo cha kumuondoa Shabani Kisiga ambaye ndiye mfungaji bora wa timu akiwa sambamba na Emmanuel Okwi wakiwa na mabao mawili kila mmoja, ni kupunguza morali ya timu.
Mtibwa Sugar wako kwenye wakati mzuri kutokana na ubora wa kikosi chao ingawa pia, wanatakiwa kuchukulia mchezo wao dhidi ya Simba kwa tahadhaari kubwa sana.
Simba watakuja wamepania kuhakikisha wanaondoka na alama tatu na kujinusuru na timua timua ambayo inanukia kwenye klabu hiyo. Mchawi wa Simba ni wanasimba wenyewe.
Huu ndiyo muda wanaotakiwa kushikamana na kuhakikisha timu inafanya vizuri na kurudi kwenye ubora wake.
Simba anaelekea kwenye mchezo huo huku akiwa kwenye nafasi ya tisa akiwa na pointi tano. Nafasi ya pili ikishikiliwa na Azam na ya nne, Yanga ambao wote wanapointi 10 ila tofauti ni magoli ya kufungwa na kufunga.
0 comments:
Post a Comment