Searching...
Image and video hosting by TinyPic
5 August 2014
Tuesday, August 05, 2014

Yanga walitakiwa kwenda kucheza Kagame.



Na Oscar Oscar Jr

Tayari kuna habari kuwa timu ya Yanga haitoshiriki michuano ya Kagame inayoshirikisha klabu bingwa kutoka nchini wanachama wa Afrika Mashariki na Kati na badala yake, mabingwa wapya wa ligi kuu Tanzania bara timu ya Azam imepewa nafasi hiyo baada ya Yanga kuenguliwa kwa madai ya kupeleka kikosi B kitu ambacho ni kinyume na kanuni za mashindano hayo.

Mashindano haya yangeweza kuinufaisha zaidi Yanga kuliko hata CECAFA. Yanga wanajiandaa kwa ajili ya ligi kuu ambayo itaaaanza kutimua vumbi septemba 20 mwaka huu, Yanga imeondokewa na wachezaji wake muhimu wa msimu uliopita Frank Domayo na Didier Kavumbagu waliojiunga na timu ya Azam lakini pia, timu hii imesajili Coutinho na Jaja kutoka nchini Brazil. 

Michuano hii ingeweza kutumika kupima ubora wa wachezaji hao wageni na kuona kama nafasi zilizoachwa na Chuji, Kavumbagu, Domayo kama zimezibika. Ndiyo maana kwenye mechi za kabla ya msimu unaona timu kama  Arsenal wamemjaribia Alexies Sanchez, Man United wamemjaribia Ander Herrera na hata Chelsea wamemjaribia Diego Coasta. 

Yanga wangeweza pia kutumia fursa hii kuona ni mchezaji gani wa kigeni wa kumtema kutokana na kanuni za TFF zinazoruhusu timu kuwa na wachezaji wa kigeni wasiozidi watano huku wao wakiwanao sita.

Maximo amewahi kuwa kwenye timu yetu ya taifa na alikuwa anawapokea kina Nizar Khalfan na Henry Joseph wakitokea nje ya nchi siku moja au mbili kuelekea mechi ya Stars na walikuwa wanacheza kwenye kikosi chake. Mchezaji wa ligi kuu hafundishwi mpira bali mbinu tu. 

Bado Maximo haitaji mwezi mzima kuwafundisha Dida au Okwi namna anavyotaka wacheza. Samatta na Ulimwengu wanajiunga kila siku na Stars dakika za mwisho na wanakiputa! Hoja ya kutokuwa na wachezaji hao muda mrefu haina mashiko.

Yanga watashiriki michuano ya shirikisho barani Afrika mwaka huu ambayo inawakutanisha washindi wa pili kwenye ligi kutoka nchi wanachama wa Caf. 

Kwenda kucheza Kagame wangeweza kukutana na mabingwa wa nchi wanachama wa Caf ukanda wa CECAFA na hii ingekuwa nafasi nzuri kwao kupata changamoto kutoka kwa wachezaji mbalimbali wenye ubora tofauti.

Wazo la Yanga kutaka kuwatumia wachezaji vijana bado lingeweza kufanikiwa tu. Yanga wangeweza kutuma kikosi chote kule Rwanda na suala la mchezaji gani aanze lingeendelea kuwa mikononi mwa kocha Marcio Maximo. 

CECAFA kamwe wasingemwingilia kwenye kupanga kikosi. Jaja na Coutinho haina haja ya kuwakumbatia utadhani wameshawahi kutwaa medali ya kombe la dunia!

Ni kweli kuna uwezokano CECAFA wanataka kuongeza mvuto wa mashindano pale ambapo Yanga ingepeleka chama lao lote lililosheheni watu wenye majina makubwa lakini kama Yanga wangekuwa makini, wao ndiyo wangenufaika zaidi. 

Wangeweza kuuza bidhaa zao, wangeweza kuandikisha wanachama huko ambao wangelipia ada kabisa na mambo mengine kibao kwa sababu wanaonekana kukubalika zaidi.

Kila siku tunalalamika kuwa wachezaji wetu hawapati mechi za kutosha kutokana na mechi chache za ligi wanazocheza  ndiyo maana wanashindwa hata kuisaidia Taifa Stars, leo hii michuano imekuja watu wanaipuuza! Yanga alistahili kushiriki michuano hii na pengine kutwaa kabisa kombe ili aanze kurudisha gharama za kumleta Marcio Maximo mwenyewe na hao wanae.


0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!